MWENENDO wa mambo ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) sasa si shwari baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kutangaza nia ya kurejea kwenye wadhifa wake huo.
Tayari ndani ya CUF viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho wamegawanyika kati ya wale wanaomuunga mkono na wanaompinga katika nia ya kuutaka tena wadhifa wa uenyekiti baada ya kujiuzulu Agosti 5, mwaka jana kwa kile alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na NCCR-Mageuzi kumpitisha Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Prof. Lipumba alitangaza nia ya kurejea katika nafasi ya uenyekiti Juni 13, mwaka huu na siku chache baadaye alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa amekwishamwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ya kutengua barua yake ya kujiuzulu.
Uamuzi huo wa Prof. Lipumba umeonekana kutoungwa mkono na baadhi ya viongozi wa CUF na tayari wapo waliokwishajitokeza kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu huku wanachama na wapenzi wa chama hicho wakiwa wamegawanyika.
Wakati hali ikiwa hivyo, jana Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Twaha Taslima, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho Buguruni na kumuonya Prof. Lipumba asijaribu kukiyumbisha chama.
Katika mkutano huo, Taslima alisema uongozi wa CUF haumwamini Prof. Lipumba ingawa unamchukulia kama mwanachama wa kawaida kupitia sera ya ‘haki sawa kwa wote.’
Taslima ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki alisema kuwa matamshi ya Prof. Lipumba ya hivi karibuni yamewachangana wanachama na mashabiki wa CUF na kwamba asithubutu kuwayumbisha kipindi hiki ambacho nchi ina matatizo makubwa na Watanzania wanahitaji kuwekwa pamoja na kupewa matumaini ya namna gani matatizo yao yanaweza kutatuliwa.
Alisema wanachama wengi wa CUF wamekuwa wakiwauliza viongozi maswali magumu likiwemo la sababu iliyomfanya Prof. Lipumba aamue kujiuzulu uenyekiti kwa kuandika barua rasmi na kwamba iwapo sababu hizo sasa zimefutwa au zimetafutiwa ufumbuzi.
Aliyataja maswali mengine yanayoulizwa na wanachama ni sababu zilizomfanya ajiuzulu haziwezi kutokea tena na kama zitatokea tena atajiuzulu kwa mara nyingine.
“Iweje Profesa Lipumba akae nje ya uongozi kwa takribani miezi kumi ndiyo leo aamue kuandika barua ya kufuta barua ya awali ya kujiuzulu? Hivi madai ya kutojibiwa barua ya kujiuzulu ndio msingi wa hoja yake ya kurudi katika nafasi ya uenyekiti? Hajui kwamba Mkutano Mkuu wa Taifa haukuhitajika kufanyika kwa ajili ya jambo hili?
“Msingi wa maswali hayo umesababisha uongozi kushindwa kuyajibu kwa ufasaha hivyo chama kinamtahadharisha Profesa Lipumba asijaribu kukiyumbisha.
“Kinyume cha hali hii wapo wananchi wengi wanaweza kujengwa na fikra kwamba hatua ya baadhi ya wanaojiita wafia CUF ambao nyakati zote wamekuwa wanapita maeneo mbalimbali kutoa kauli za uongo kwa lengo la kuwagawa viongozi wa chama na wanachama na wamekwishabainika wanatumiwa na maadui kwa lengo la kudhoofisha chama inaweza kuonekana kwamba yana baraka yake na hivyo kushusha heshima yake kwa jamii,” alisema Taslima.
Hata hivyo, Taslima alisema kuwa Prof. Lipumba anayo nafasi ya kugombea uenyekiti au kuwania nafasi yoyote ya uongozi kama ilivyo kwa wanachama wengine ambao watachukua fomu.
Alisema uchaguzi wa kuziba mapengo katika nafasi mbalimbali za uongozi utafanyika wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho Agosti 21, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Abubakari Khamis Bakar, ambaye pia alipata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo alinukuu ibara ya 31;1 ya Katiba ya chama hicho inayoeleza kuwa mwanachama yeyote anao uhuru wa kujiuzulu katika wadhifa wowote wa uongozi.
Alisema Prof. Lipumba alichukua uamuzi wa kujiuzulu baada ya kuzingatia ibara hiyo ya katiba hivyo hawezi kutengua uamuzi wake wa awali kwa sababu alifuata utaratibu wa kikatiba.
Bakar alisema Prof. Lipumba alijiuzulu uongozi wakati chama kikiwa katika wakati mgumu wa hekaheka za uchaguzi mkuu lakini Mungu alinyoosha mkono wake chama hicho kikafanikiwa kupata wabunge 10 na halmashauri tano.
“Profesa amekuwa kiongozi kwa muda mrefu lakini hajawahi kufanikiwa kupata viti vya ubunge kama ilivyo sasa, binafsi napenda kusema kwamba sisi tuna miguu mirefu zaidi ya viatu chake,” alisema Bakar
Awali katika mkutano huo, Taslima alitangaza mpango wake wa kuwania nafasi ya uongozi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Agosti 21.
“Ndani ya miezi 10 tangu nilipopewa dhamana ya kuongoza kamati ya uongozi wa chama kuna mambo mengi nimejifunza na kuelewa, naona ni bora na mimi nikavuta fomu ili nigombee nafasi ya uenyekiti katika mkutano wa Agosti 12,” alisema Taslima.
Prof. Lipumba alitangaza kurejea kwenye nafasi yake Juni 13, mwaka huu kwa maelezo kwamba amechukua hatua hiyo baada ya muda wa kutosha alioutumia kutafakari siasa za hapa nchini na namna demokrasia inavyokanyagwa na watawala.
“Nimemwandikia Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) kutengua barua yangu niliyoandika Agosti 5, mwaka jana.
“Katiba ya chama ya mwaka 1992, Toleo 2013 Ibara ya 117 inaeleza kwamba, barua ya kujiuzulu inapaswa kujadiliwa na Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika,” alisema Prof. Lipumba.
Alisisitiza kuwa analazimika kurejea kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa kutokana na kuguswa na matatizo ya demokrasia nchini.