Na ELIZABETH HOMBO-DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema mambo ya mila, desturi na itikadi hayataki haraka hivyo ni vigumu kuyabadili kwa kutumia sheria pekee.
Profesa Kabudi alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), aliyetaka kujua ni kwanini asilete muswada bungeni kuhusu suala la kifungu cha 13 na 17 cha sheria ya ndoa, ili amri hiyo ya mahakama ya rufaa itekelezwe kwa watoto wa kike na wa kiume kupata haki ya kusoma na kuwa viongozi wa taifa hilo.
“Kwa kuwa mheshimiwa waziri ambaye ni mwalimu wangu nampongeza sana kwa majibu mazuri kama hawatamharibu ataenda vizuri sana, kwa sababu waziri amekiri kwamba yeye mwenyewe kama mzazi na kama mwalimu umri wa mtoto wa kuoa wa miaka 14 hakubaliani nao na umri wa mtoto wa kike kuolewa wa miaka 14 hakubaliani nao pia,” alisema.
Profesa Kabudi alisema yeye anatoka katika utamaduni ambao umekuwa na mila si nzuri ya ukeketaji, sheria ipo imezuia lakini kwa sababu bado ni suala la imani na itikadi kwa watu, hivi sasa wamelihamishia kwa watoto wachanga.
“Sasa nazungumza kama profesa wa sheria ni hatari na mheshimiwa rafiki yangu mkubwa anajua kabisa kuna mila na desturi za anakotoka leo mimi siafikiani nazo lakini zinahitaji elimu na uelewa.
“Ni vigumu sana mtu anayetoka nje ya eneo hilo kuelewa kwamba mapenzi ni pamoja na kipigo, nimsihi ndugu Waitara tukae nje tukutane. Nasema masihara haya kwa kuwa ni mtu tumeshibana hawezi kunichukulia tofauti.
“Mambo ya mila na desturi, imani za dini na kiitikadi hayataki haraka bali yanataka mwafaka, kuna umuhimu huwezi kubadili mila, desturi imani ya dini na itikadi kwa kutumia sheria peke yake tu, utakuwa unajidanganya,”alisema.
Awali katika swali jingine la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alihoji ni lini Serikali itatekeleza agizo la Mahakama Kuu, kuhusu hukumu waliyoitoa ya kifungu cha 13 na 17 kwenye suala la sheria ya ndoa ili kukifuta kifungu hicho.
Akijibu swali hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema baada ya maamuzi yale Serikali ilikata rufaa na kwa mujibu wa sheria pale tu kama ni kesi ya kikatiba unapowasilisha waraka wa kukata rufaa inasimamisha utekelezaji moja kwa moja wa maamuzi ya Mahakama.
Masaju alisema kesi ile haikuwa na mambo ya ndoa pekee na kwamba kuna mambo mengi yalijitokeza, hivyo ni lazima wapate mwongozo wa Mahakama ya Rufaa.
Awali katika swali lake la msingi, Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM), alitaka kujua ni lini Serikali italeta hoja ya kufanya marekebisho ya kuboresha baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati.
“Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya sheria zetu hapa nchini zimekuwa haziendani na kazi ya maendeleo ya taifa na kuonekana kuwa zimepitwa na wakati,”alisema.
Mulugo alisema, ipo sheria ya ndoa ambayo inasema mtoto mwenye umri wa miaka 14 anaweza kuolewa, lakini yeye amekuwa mwalimu wa muda mrefu anajua, miaka 14, kwa sheria ya elimu msingi ilivyo hivi sasa anakuwa bado yupo kidato cha pili, elimu msingi chekechea hadi kidato cha nne.
Akijibu maswali hayo, Waziri Kabudi alisema kuhusu suala la sheria ya kuruhusu Bunge liwe na tume yake liko nje ya mamlaka na uwezo wake kwa kuwa hilo ni suala la Bunge lenyewe.
Alisema sheria za nchi hubadilika kulingana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kisayansi na kiteknolojia.
“Mabadiliko yanayojitokeza yanaweza kuathiri sheria zilizopo na hivyo kuonekana kuwa zimepitwa na wakati au kuwa na upungufu hivyo kutokidhi matakwa ya wakati,” alisema.