Banjul, Gambia
Mtoto wa malikia wa Uingereza, Queen Elizabeth II na mrithi wa kiti cha Ufalme, Prince Charles pamoja na mke wake Camilla, wamewasili nchini Gambia Jumatano ya jioni ya Octoba 31,2018.
Wanandoa hao wapo katika ziara ya wiki moja huko Afrika Magharibi, katika kudumisha uhusiano na nchi washirika wa jumuiya ya madola.
Charles na mkewe Camila, wamewasili Uwanja wa ndege wa Banjul jioni jana na kupokelewa na Rais Adama Barrow na mkewe, Fatou Bah-Barrow.
Katika ziara yake ya kwanza nchini Gambia, Prince Charles leo atatembelea Baraza la Utafiti wa Matibabu huko Banjul ambacho ni kituo maalumu cha kupambana na malaria.
Ijumaa Prince Charles na mkewe wanatarajiwa kwenda nchini Ghana na ziara yao itakamilika nchini Nigeria, Novemba 6 hadi 8.
Prince huyo amesema safari yake Afrika Magharibi, inalenga kusherehekea ushirikiano wa nguvu na endelevu wa Uingereza na nchi hizo za Jumuiya ya Madola.
Gambia ni nchi ndogo ya Afrika Magharibi, inayozungumza Kiingereza ilirejeshwa tena katika Jumuiya ya madola mwezi februari baada ya kujitoa ghafla katika Jumuiya hiyo mwaka 2013.