Na Grace Shitundu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Ndege la Precision linatarajia kuuza baadhi ya ndege zake na kubakiza ndege sita kupunguza mzigo wa madeni yanayoikabili Kampuni hiyo kwa sasa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Michael Shirima alisema Dar es Salaam jana kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na uchakavu wa ndege hizo na hali ya uchumi wa kampuni.
“Kampuni iko katika mazungumzo na mwekezaji ili kukamilisha makubaliano ya kununua ndege zenye madeni na kisha kuzikodisha kwa kampuni nyingine… makubaliano haya yanatarajiwa kufikiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka huu,” alisema Shirima.
Alisema pamoja na kufikia hatua hiyo kampuni haijakata tamaa kwa kuweka jitihada ya kutafuta mtaji mkubwa kupitia kwa wanahisa wa sasa au wawekezaji wasio wanahisa.
Awali akiitoa taarifa katika mkutano mkuu wa mwaka wa Tatu wa wanahisa, Shirima alisema mazingira ya biashara yalikuwa na ushindani huku kukiwa na hofu juu ya usalama duniani kote.
Pia alisema thamani ya fedha za kigeni hususan Dola ya Marekani imeendelea kukua ikilinganisha na shilingi ya Tanzania hivyo kusababisha akiba hafifu ya fedha za kigeni na hasara kwa biashara ambazo matumizi yake mengi yanategemea fedha hizo.