JOHANES RESPICHIUS NA FERDNANDA MBAMILA- DAR ES SALAAM
MFUKO wa Pensheni (PPF) umeanza kufanya uhakiki wa wanachama wake waliofikia umri wa kustaafu ili kuwatambua wanaostahili kulipwa mafao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja Kiongozi wa Shughuli za Pensheni na Huduma kwa Wanachama, John Mwalisu, alisema lengo la uhakiki huo ni kutambua wanachama wenye sifa ya kulipwa.
Alisema uhakiki huo ulianza Septemba 12 mwaka huu na utamalizika Oktoba 28, ukihusisha mikoa yote ikitanguliwa na Dar es Salaam, Pwani, Zanzibar na Tanga na itafuatiwa na Arusha, Mwanza, Morogoro na Mbeya.
“Utaratibu wa kuhakiki wastaafu huwa unafanyika kila baada ya miaka miwili lengo likiwa ni kuweka kumbukumbu sahihi za wastaafu wanaopewa pensheni kila mwezi,” alisema Mwalisu.
Aidha, alisema PPF imezindua fao jipya la kujifungua na mfumo wa Wote Scheme wenye lengo la kukidhi mahitaji ya kutambua michango ya ushiriki wa sekta isiyo rasmi kiuchumi.
“Wote Scheme inatoa fursa kwa wafanyakazi walio kwenye sekta isiyo rasmi ili kuwawezesha kunufaika na mfumo huu kwa ajili ya kukuza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
“Sekta hii haifungamani na Serikali kwa sababu si rasmi, kwa maana hiyo inalenga kila mtu au kikundi chenye kipato cha kawaida kilicho na mlengo wa kiuchumi katika sekta isiyo rasmi kama wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, mama lishe, wasanii, wanamichezo, wachimbaji madini wadogo, bodaboda na wajasiriamali wadogo,” alisema Mwalisu.
Alitoa wito kwa wananchi kujiunga na mfuko huo ili kujiwekea uhakika wa maisha bora ya uzeeni.