BAGHDAD, IRAQ
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema Serikali ya Iraq inapaswa kuyasikiliza madai halali ya watu wanaoandamana kupinga rushwa na ukosefu wa ajira.
Pompeo amesema Marekani inafuatilia kwa karibu hali nchini Iraq.
Katika taarifa yake, mwanadiplomasia huyo amesema uchunguzi wa Iraq kuhusu ghasia zilizozuka mwanzoni mwa mwezi Oktoba, haukuwa wa kuaminika na kwamba watu wa Iraq wanastahili kupata haki ya kweli. Wakati huo huo, kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatollah Ali al-Sistani, ameonya kuhusu mataifa ya kigeni kuingilia maandamano yanayoendelea ya kuipinga serikali.
Al-Sistani amesema Iraq haipaswi kutumbukizwa kwenye shimo la mauaji.
Matamshi hayo yametolewa siku moja baada ya kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei kuzitaka Iraq na Lebanon kulifanya suala la usalama kuwa kipaumbele chao.