JESHI la Polisi Visiwani Zanzibar limezuia dhamana ya mwanamkakati wa aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kutokana na tuhuma zinazomkabili.
Mwanamkakati huyo ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Mohammed Ahmed Sultan, maarufu Eddy Riyami, anatuhumiwa kutoa lugha ya matusi kwenye mitandao ya jamii.
Akizungumza na MTANZANIA mjini Unguja jana, mmoja wa wanasheria wa Riyami ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema Jeshi la Polisi limezuia dhamana ya kiongozi huyo.
“Hadi sasa bado Jeshi la Polisi limeendelea kuzuia dhamana kwa Eddy Riyami, lakini mimi kwa kushirikiana na wanasheria wengine tunafanya jitihada suala hili lifikishwe mahakamani,” alisema mwanasheria huyo.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Salum Msangi, alisema wanaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo na watatoa taarifa zaidi kwa vyombo vya habari uchunguzi utakapokamilika.
Wakati hayo yakiendelea, CUF kimetoa taarifa kikisema hadi sasa hayajapatikana maelezo ya msingi kuhusu kinachoendelea kuhusu suala la Riyami.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Hamad Masoud Hamad, alisema hatua ya Jeshi la Polisi kuendelea kumshikilia mjumbe wa timu ya kampeni ya chama hicho, ni mwendelezo wa vitendo vya unyanyasaji wa siasa kwa wapinzani wa CCM.
Alisema kukamatwa kwa mjumbe huyo ni shinikizo linalofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa visiwani Zanzibar jambo ambalo si sahihi katika ujenzi wa demokrasia.
“Na jambo la ajabu zaidi hata mke wake alipokwenda makao makuu ya jeshi hilo hakuruhusiwa kuonana na mume wake jambo ambalo si la ustaarabu na utu.
“Ni vema sasa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa utaalamu kama sheria na kanuni zao zinavyoagiza badala ya kuwatumikia wanasiasa,” alisema Masoud.