26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Madudu ya ufisadi Manispaa Ilala

kuyekoNA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

MANISPAA ya Ilala, Dar es Salaam imeanza ukaguzi wa ndani ili kubaini ufisadi katika mfumo wa ulipaji mishahara ya askari mgambo.

Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa baadhi ya mgambo hao walikuwa wakilipwa mshahara tofauti na uliokuwa unafahamika wa Sh 280,000 kwa mwezi.

Badala yake baadhi yao walikuwa wakilipwa kati ya Sh 50,000 na 80,000 kama posho badala ya Sh 280,000 zilizokuwa zimeidhinishwa na manispaa hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kukabidhiwa Ilani ya Ukawa pamoja na mwongozo wa kazi, Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, alisema  baadhi ya maofisa ambao si waaminifu walikuwa wakijichotea fedha kupitia mishahara ya mgambo kinyume cha sheria.

Alisema Manispaa ya Ilala ilikuwa na mgambo 150 ambao walikuwa wakiajiriwa kwa mkataba wa miezi mitatu, lakini watendaji walikuwa wakitumia mbinu chafu kuwapunja mishahara yao.

“Katika uchunguzi wetu tumebaini mgambo hao baada ya kumaliza mkataba wa miezi mitatu walikuwa wakipunguzwa na kubaki 100, huku 50 wakiondolewa kwenye ajira, lakini vitabu vya mishahara vilionyesha ni 150.

“Walikuwa wakisimamishwa kazi huku wakiendelea kuwatumikisha kwa ujanja bila kuwapa malipo yao stahiki, wakati vitabu vya manispaa vilikuwa vikionyesha wanalipwa mshahara kamili.

“Cha ajabu baada ya ukaguzi wa awali tulibaini baadhi ya mgambo walikuwa wakisitishiwa mkataba na kutumiwa kwa ujanja kisha kulipwa Sh 50,000 hadi 80,000 wakati kwenye vitabu vya manispaa vilikuwa vinaonyesha wamelipwa Sh 280,000 ambazo walikubaliana awali,” alisema Kuyeko.

 MABANGO YA BIASHARA

Kuyeko alisema Manispaa ya Ilala imeingia mkataba na kampuni ambayo imeanza kufuatilia mabango yote yaliyokuwa yanakwepa kulipiwa ushuru pamoja na kodi kwa ujumla.

Aidha Kuyeko alizungumzia hali mbaya iliyopo katika miundombinu ya elimu ambapo alisema shule nyingi za Serikali zipo hoi kiasi cha kukatisha tamaa.

Alizitaja shule za sekondari Azania, Pugu Bangulo, Pugu Stesheni na Bonyokwa kuwa miundombinu yao imechakaa kiasi cha kutisha na kuhatarisha maisha ya walimu na wanafunzi.

Akitolea mfano Shule ya Bangulo, alisema darasa la kwanza lina wanafunzi 305, huku kila moja likiwa na wanafunzi 100, hivyo walimu wanalazimika kufundisha chini ya miti kutokana na uhaba wa madarasa.

Alisema katika Sekondari ya Azania wameshuhudia vyoo vikiwa vimefurika maji taka na wanafunzi wanalala chini kutokana na msongamano kuwa mkubwa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Kuyeko alisema wameweka mkakati wa kujenga madarasa matano kila shule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles