Sarah Mossi na Grace Shitundu, Dar es Salaam
UCHUNGUZI uliofanywa na Jeshi la Polisi nchini juu ya kifo cha Balozi wa Libya nchini, Ismail Hussein Nwairat (39) umebaini hakuna dalili zinazoonyesha kama aliuawa.
Polisi juzi walilazimika kufanya uchunguzi wa tukio hilo la kujipiga risasi balozi huyo lililotokea Julai mosi mwaka huu saa 7:15 mchana katika ofisi za ubalozi zilizopo Mtaa wa Mtitu, Upanga jijini Dar es Salaam.
Tukio la kujiua kwa balozi huyo liliacha maswali mengi ikiwamo sababu za kujiua na baadhi ya wadadisi wa masuala ya kidiplomasia wakidai pengine aliuawa.
Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania uliwahusisha wataalamu wa kuchunguza vifo vya aina hiyo kwa kushirikiana na maofisa wa Ubalozi wa Libya pamoja na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
“Staili aliyotumia ni kujishuti, hakuuawa, huo ndio uchunguzi wetu tulioufanya leo (juzi), umebaini,” kilisema chanzo cha habari kutoka Polisi Makao Makuu.
Chanzo cha habari kutoka Makao Makuu ya Polisi nchini kilisema jana kuwa kabla ya kutekeleza tukio la kujiua, Balozi huyo aliacha ujumbe aliotaka uende kwa watoto wake wawili wakike na wa kiume.
Kwa mujibu wa chanzo hicho ujumbe huo ulioandikwa kwa lugha ya Kiarabu ulisomeka hivi:
“Kwa jina la Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, mwenye kurehemu, Sanad Ismail Hussein, Mohmed Nwairat, Mayas Ismail, Hussein Nwairat, Ewe Mola wangu awahifadhi”.
“Juzi tumepata kibali cha kufanya uchunguzi na tumeingia ndani ya ofisi katika kiti chake tumekuta bastola na karatasi yenye maneno ya Kiarabu.
“Tukatafuta mkalimali wa lugha hiyo na ametutafsiria ujumbe alioacha kwenda kwa watoto wake, ndio huo niliokupa,” kilisema chanzo hicho.
Balozi Nwairati alijiua kwa kujipiga risasi akiwa amejifungia ndani ya ofisi za ubalozi wa Libya, Julai mosi mwaka huu saa 13:15 mchana huku chanzo cha kuchukua uamuzi huo kikiwa hakijafahamika.
Wakati huo huo habari zilizopatikana jana jioni zilisema mwili wa Balozi Ismail Mwairat umesafirishwa jana usiku kupelekwa Libya kwa mazishi.
Habari zilizopatikana kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilisema mwili huo ulisafirishwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Egypt saa saba usiku.
Habari hizo zilisema taratibu zote za kuusafirisha mwili huo zilifanywa na ofisi ya Ubalozi wa Libya nchini.