28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waliotimuliwa kwa tuhuma za wizi MSC waajiriwa upya

meli mwanza
meli mwanza

Na Mwandishi Wetu, Bukoba

WATUMISHI watatu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC) wanaodaiwa kuwahi kuhusika na wizi wa fedha za umma na kutimuliwa kazini wameajiriwa tena.

Hatua hiyo imekuwa ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuamuru watumishi 13 wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuondolewa kazini kwa madai ya kula rushwa.

Wafanyakazi hao wameajiriwa upya kuanzia Julai 17, 2012 na Machi 7, 2013 kwa madai ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali licha ya kudaiwa walihusika na upotevu wa mamilioni ya fedha za kampuni hiyo ya meli ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Uchukuzi.

Wafanyakazi hao ni Fasso Obondi akiwa Karani Daraja la II (Traffic Clerk II), Magayane Walu akiwa ni Karani Daraja la III na Jacob Kimwaga aliyekuwa Karani Utumishi (Personal Clerk). Wamerejeshwa kazini katika nafasi zao za awali.

Wafanyakazi hao walitimuliwa kazi kwa vipindi tofauti kwa makosa ya wizi wa fedha za kampuni wakati wakiwa Tawi la Kigoma chini ya Meneja Biashara, Projest Kaija, ambaye sasa ni Meneja Mkuu wa MSC.

Ajira za wafanyakazi hao zinadaiwa kuzua mvutano baina ya Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo na maofisa wengine ikidaiwa ni kinyume na sheria za kazi kwa vile tayari waliondolewa kwa makosa ambayo ni makubwa yasiyostaili kurudishwa kazini.

Obondi amepewa mkataba unaomalizika Machi 6 mwaka huu, wakati Kimwaga mkataba wake ulimalizika Julai 8  mwaka jana na kuongezewa sambamba na Walu aliyepewa mkataba mpya baada ya mkataba wake wa awali kumalizika Julai 16 mwaka jana.

Jacob Kimwaga akiwa Karani wa Utumishi alituhumiwa kuhusika kuwapanga zamu za kwenda na meli makarani kwa upendeleo huku akiwaacha watumishi wengine hatua iliyohusishwa na rushwa nakusababisha ubadhirifu wa fedha.

Hata hivyo hakuna ushahidi wa moja kwa moja uliopatikana katika tuhuma hizo, lakini mkataba wake ulisitishwa mwaka 2010.

Obondi alitimuliwa kazi Aprili 25, 2007 na kulipwa haki zake zote kiasi cha Sh milioni 2.7 kwa hundi namba 008429 (Sh 170,453), hundi namba 008431 (Sh 976,420.00) pamoja na hundi namba 008430 (Sh 1,558,054.55).

Kwa mujibu wa nyaraka za shauri la Obondi C/No 651022 lenye kumbukumbu namba MAC MEMO MSC/D/02/2005, alifukuzwa kwa kuhusika na upotevu wa dola za Marekani 510 baada ya kuwasilisha kwa mwajiri wake dola 425 badala ya dola 935 zilizolipwa na Kamanga Group wa Spanish Tourist.

Dola hizo 935 zilikuwa ni malipo ya Watalii 17 waliokuwa wakisafiri kutoka Kigoma kwa meli ya MV. Liemba kwenda Mpulungu kwa tiketi namba 067028 lakini Obondi alionyesha kuwa watalii hao walisafiri umbali mfupi kutoka Kigoma kwenda Lagosa kwa tiketi namba 164095 za daraja la kwanza yenye abiria wa daraja la tatu na wengine 14 tiketi namba 164095 daraja la kwanza, hiyo ilikuwa ni kati ya Oktoba 16 na 20, 2002.

Makosa mengine yaliyomkabili ni pamoja na kutoa mawakilisho ya mauzo ya tiketi kidogo ikilinganishwa na inavyotakiwa ambapo alipotakiwa kuwasilisha nyaraka za ofisi kwa wakaguzi wa MSC Tawi la Kigoma zilizokuwa zikionesha mauzo ya idadi ya tiketi, idadi ya abiria, vituo walivyosafiri na madaraja yao kuanzia Oktoba 2, 2002 hadi Januari 15, 200.

Katika tiketi za SFT namba TU 067144 mpaka TU 067150 ambazo zilitolewa Januari mosi 2003 zenye makusanyo ya Sh 86,000 aliweza kuwakilisha kiasi cha Sh 19,800 kwa mwajiri na Sh 66,200 hazikuwasilishwa, Januari 2, 2003 Tiketi (SFTS) namba TT 209138 mpaka 209141 zenye makusanyo ya Dola 440 pesa aliyopeleka benki ilikuwa ni dola za Marekani 285 na kudaiwa kuweka mfukoni mwake dola za Marekani 155.

Kwa upande wake, Magayane Walu nyaraka za shauri lake C/No 038321 lenye kumbukumbu Office Memo namba MSC/05/2009, anadaiwa akiwa karani katika meli ya MV. Mwongozo iliyopo Tawi la Kigoma, alishindwa kuwasilisha benki Sh milioni 4.9 ikiwa ni fedha za mauzo ya tiketi pamoja na kuhusika na upotevu wa vitabu vya tiketi SFT namba 373601, 50K, 373651, 373700 zote ni za Mei 21, 2008.

Ilidaiwa kwa kipindi cha siku 21 kuanzia Desemba 29, 2007 hadi Januari 10, 2008, Walu alipaswa kuwasilishwa benki kwa mwajiri kiasi cha Sh 2,015,500 (010676), Januari 4 hadi 19, 2008 awasilishe kiasi cha Sh 1,849,500 (010677), Machi 14 hadi 29, 2008 awasilishe Sh 972,000 (010685) na Aprili 11 hadi 26, 2008 alipaswa kuwasilisha benki Sh 144,975 (010689) lakini hakufanya hivyo na kumtia hasara mwajiri wake.

Meneja Mkuu wa MSC, Projest Kaija alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alikanusha kuwarejesha kazini wafanyakazi hao kwa misingi ya upendeleo na kusisitiza wafanyakazi hao  wamerejeshwa kutokana na maelekezo yaliyotoka ngazi za juu kutokana na ufanisi wao kazini.

“Unajua kuna wafanyakazi tuliwatimua hapa, sasa hawa walikuwa wakijihusisha na wizi wa fedha, nadhani ndiyo ambao wameamua kunichafua kwa visingizio hivi na vile, lakini mimi ni muadilifu nitaendelea kusimamia misingi ya kazi na uwajibikaji,” alieleza Kaija.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles