NA HADIA KHAMIS – DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Mkoa wa kipolisi wa Temeke kwa kushirikiana na wenzao wa Mkoa wa Pwani wamewaua majambazi wanne.
Tukio hilo limetokea wakati Agosti, mwaka huu, Kikosi Maalumu cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Uhalifu kilipambana na majambazi waliokuwa wakiishi katika nyumba iliyopo eneo la Vikindu wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani na askari mmoja alipoteza maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto, alisema katika mapambano hayo majambazi watano walifanikiwa kutoroka sehemu isiyojulikana.
Kamanda Muroto alisema walipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamejificha katika Kijiji cha Mtambani, Kata ya Tambani wilayani Mkuranga.
Kutokana na taarifa hiyo, alisema kikosi kazi cha polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kilifuatilia na kubaini nyumba ambayo ujenzi wake ulikuwa haujaisha, ikiwa imezungushiwa uzio na muda wote mlango wake ulikuwa unafungwa.
“Uchunguzi wa kina ulifanyika na kubaini kuwa kweli kundi hilo lipo ndani ya nyumba hiyo na muda mwingi mlango ulikuwa unafungwa,” alisema Kamanda Muroto.
Pia alisema saa tano na nusu usiku, askari hao na wenzao wa Pwani walizingira nyumba hiyo na baada ya kujipanga, mlango wa uzio huo uligongwa na kutoa amri ya kuwataka waliomo ndani wafungue na kujisalimisha.
Alisema baada ya amri hiyo kutolewa, ghafla milio ya risasi ilianza kutoka ndani ya nyumba hiyo na kuwalazimu askari waliojipanga katika muundo wa mapigano kujibu shambulio hilo.
Kamanda Muroto alisema majibizano yaliendelea na watu hao waliokuwa wanashambulia kutoka ndani walivunja uzio na kuendelea kuwashambulia.
“Askari waliendelea kupambana nao na kufanikiwa kuwajeruhi na baadhi ya majambazi walifanikiwa kutoroka na silaha zao, mashambulizi toka ndani yalitulia na askari waliingia ndani ambako walikuta majambazi watatu waliojeruhiwa na hali zao zikiwa mbaya,” alisema Kamanda Muroto.
Alisema waliipekua nyumba hiyo na walifanikiwa kupata bunduki moja aina shot-gun yenye namba MV.51516R na usajili TZcar 99987 ikiwa na risasi tano ndani ya magazine yake na risasi nyingine sita zilipatikana ndani ya mfuko wa rambo pamoja na risasi nane za bastola.