25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WANAODAIWA KUIBA MAFUTA YA NDEGE WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


ASKARI wawili wanaotuhumiwa kuiba mafuta ya ndege ya Kampuni ya ATCL, kwa kushirikiana na walinzi, wameondolewa kazini na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao na wenzao wawili walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.

Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Koplo Bahati Msilimini (33), PC Benaus (34), Iddi Nyangasa (42) na fundi wa ndege, Ramadhani Mwishehe (52).

Katuga alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka  mawili, shtaka la kwanza kula njama na shtaka la pili hujuma dhidi ya Serikali.

Alidai katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi mosi na Machi 17 mwaka huu maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere walikula njama ya kutenda kosa la uhujumu uchumi.

Katika shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa kati ya tarehe hizo, wakiwa na nia ya kuhujumu manufaa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, bila uhalali walitoboa na kuchota mafuta ya ndege lita 280.6 kutoka kwenye ndege JET A1 ya ATCL yenye namba za usajili 5H\MWF-8Q-300.

Katuga alidai kitendo hicho kilizuia utoaji wa huduma muhimu ya usafiri wa ndege.

Hata hivyo wakili huyo alidai upelelezi haujakamilika na hakuna kibali chochote kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Wakili wa utetezi, Martin Rwehumbiza aliiomba mahakama ikubali kuwapa dhamana wateja wake kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhamana.

Alidai thamani ya mafuta wanayodaiwa kuchota haizidi Sh milioni 10 hivyo mahakama hiyo ina mamlaka ya kutoa dhamana.

Akijibu hoja hiyo Katuga alipinga washtakiwa hao kupewa dhamana kwa madai kwamba wataingilia upelelezi hivyo aliomba wakae ndani kwa muda.

Akitoa uamuzi Hakimu Nongwa alisema sheria inaruhusu Mahakama ya Kisutu kushughulikia dhamana kwa makosa mbayo thamani yake haizidi Sh milioni 10.

“Sirahisi kujua mafuta yalikuwa na thamani gani sababu hayakuwekwa katika hati ya mashtaka, hakuna hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa DPP, wangeona washtakiwa wakiwa nje kwa dhamana wataingilia upelelezi wangeweka hati ya kuzuia dhamana zao.

“Dhamana ni haki ya washtakiwa hakuna zuio lolote, mahakama inaona ni vyema washtakiwa wakapewa dhamana, hawawezi kuingilia upelelezi sababu walishaondolewa kazini,”alisema Hakimu Nongwa.

Washtakiwa wote walipata dhamana na wadhamini walitakiwa kuhakikisha washtakiwa hao wanafika mahakamani kila kesi itapokuwepo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 27 mwaka huu kwa kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles