27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wamdanganya Waziri Mwigulu

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MAOFISA wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Geita wamemdanganya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kuhusu ukweli wa tukio la kushambuliwa kwa Masanja Shilomero (25) na mwajiri wake ambaye ni raia wa China.

Maofisa hao walimdanganya Waziri Mwigulu ambaye alikwenda mkoani Geita kufuatilia taarifa za kunyanyaswa kwa Masanja ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyamitondo, Tarafa ya Butundwe wilayani Geita, kwa kuhofia kuwa akiujua ukweli atawatumbua.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka vyanzo vyake vya kuaminika vilivyo ndani ya jeshi hilo zimeeleza kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Wilaya ya Geita (OC-CID), Samweli Kijanga, alikwenda eneo la mgodi akiwa ameambatana na baadhi ya makachero muda mfupi baada ya kuteswa na walinzi na kukutana na uongozi wa mgodi huo.

Julai 6, mwaka huu, Masanja alipigwa na mwajiri wake aliyetambuliwa kwa jina moja la Myo ambaye ni raia wa China baada ya kuomba kupandishiwa mshahara.

Baada ya kupigwa alikamatwa na polisi ambao walimpeleka mahakamani wakiwa wamemfungulia kesi yenye namba CC 278/2016 akituhumiwa kwa kosa la wizi wa mawe.

Tukio hilo lilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kumfikia Waziri Mwigulu ambaye alifika mkoani Geita Julai 27 na kukutana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kabla ya eneo la mgodi lililo katika Kijiji cha Nyamahuna na baadaye alikwenda gerezani kukutana na Masanja.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, Kachero Kijanga na timu yake walimkamata Masanja aliyekuwa amejeruhiwa kwa kipigo na kumweka korokoro ya kituo kidogo cha polisi ya Katoro na siku iliyofuata alifikishwa Mahakama ya Mwanzo ya Katoro bila kufikishwa hospitali kwa ajili ya hati ya matibabu (PF3) wala kuchukuliwa maelezo kuhusu unyama aliofanyiwa.

Mmoja wa makachero waliopo mkoani Geita, amelieleza gazeti hili kuwa haiingii akilini kumuona Waziri akiwa na ujuzi wa kuhoji na kubaini dosari akiwazidi polisi ambao wamesomea kazi hiyo.

“Waziri kaja kahoji kwa dakika na kubaini kuna kosa la shambulio dhidi ya anayedaiwa kuteswa na Wachina, kwanini polisi wasigundue?

“Wao upelelezi uliishia kumpeleka mahabusu kwa maelezo ya mlalamikaji na hiyo ilikuwa baada ya OC-CID kukaa faragha na Wachina ambao ni wamiliki wa mgodi huo na walipomaliza kikao chao tulishuhudia kijana wa watu anakamatwa na ikaamuriwa asipewe PF3.

“Alikuwa ameumizwa sana lakini polisi hawakuona hilo wala haja ya kuita mashuhuda wa tukio na kuwahoji tofauti na waziri ambaye kwa muda mfupi aligundua uwepo wa Wachina zaidi ya 50 kinyume cha sheria, lakini tusimlaumu mkuu wa upelelezi maana tunasikia ni maagizo kutoka juu,” alisema polisi huyo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baada ya polisi kupata taarifa kuwa Waziri Mwigulu atafika Geita kufuatilia suala hilo, Julai 27, majira ya alfajiri askari polisi wawili ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa wakiwa na Kachero Kijanga walikwenda Gereza la Geita kuomba kuchukua maelezo ya Masanja.

Kwamba polisi hawakuwa na kibali cha kumtoa Masanja gerezani hivyo waliruhusiwa kuchukua maelezo yake wakiwa ofisi za gereza ili kuepuka kutumbuliwa lakini ingetokea Waziri Mwigulu akaitisha jalada la uchunguzi lililofunguliwa dhidi ya Wachina hawakuwa nalo.

Polisi mwingine wa mkoani Geita aliyezungumza na gazeti hili (jina lake tunalihifadhi kwa sababu si msemaji) alieleza kuwa makachero hao walipotoka kuchukua maelezo ya Masanja gerezani ikiwa ni muda mfupi kabla ya waziri kufika, walikwenda kufungua jalada namba GE/RB/5498/2016 la shambulio la kudhuru mwili, mlalamikaji akiwa kijana huyo ambaye mbali na kuumizwa hakupatiwa hata fomu ya matibabu (PF3) na mlalamikiwa akiwa Myo.

“Waziri akiomba jalada hilo hata leo hawabaki kwa sababu litaonyesha ni lini limefunguliwa na atabaini kuwa Masanja alipelekwa gerezani akiwa hana PF3 ambalo nalo ni kosa,” alisema polisi huyo.

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Ratson, kuhusu jambo hilo alisema hawezi kutoa taarifa kwa mtu ambaye hamfahamu licha ya kuelezwa mapema kuwa anazungumza na Gazeti la MTANZANIA.

“Mimi siwezi kuzungumza na mtu ambaye simfahamu kwa sababu taarifa nitakazotoa zina athari kwa jamii kama mna mwakilishi wenu huku mwambie aje kuniona ofisini,” alisema Afande Ratson kisha akakata simu.

Takribani wiki moja sasa kumekuwa na hali ya sintofahamu dhidi ya picha zinazoenezwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zikionesha raia wa Tanzania, Shilomero akiteswa na kufanyiwa vitendo vya kinyama na mwajiri wake ambaye ni raia wa China.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles