28.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 3, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wageuza sukari dili

sukariJONAS MUSHI NA TUNU NASSORO, DAR

WAFANYABIASHARA   Dar es Salaam wamewalalamikia baadhi ya polisi kuwanyanyasa kwa kisingizio cha kutafuta sukari iliyofichwa.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, wamiliki wa maduka ya jumla yaliyopo Kitumbini Manispaa ya Ilala, walisema wamekuwa wakipata  usumbufu huo kutoka kwa askari hao tangu kuanza   msako wa sukari inayodaiwa kufichwa na wafanyabiashara.

Mfanyabiashar, Albert Ndembuka, alisema hivi karibuni alivamiwa na askari wanne ambao  walimpekua kwa madai kuwa ameficha sukari.

“Vyombo vya usalama wamefanya tatizo hili ni fursa kwao kujipatia fedha haramu,” alisema Ndembuka na kuongeza:

“Sifanyi kazi kwa raha kwa sababu ya usumbufu mkubwa ninaopata kutoka kwa askari ambao wamekuwa wakinivamia hadi nyumbani kutaka kunipekua kwa sababu ya kuuza sukari”.

Mfanyabiashara Mtaa wa Aggrey Kisutu, Geofrey Peter,  alisema askari wanawasababishia usumbufu mkubwa kwa kukamata sukari wakati wakiisafirisha kutoka kwenye maghala kuipeleka madukani kwa madai ya kuikagua.

“Usumbufu ni mkubwa, kuna watu juzi walikamatwa wakiwa wametoka kununua sukari wakiwa na vibali vyao mkononi lakini askari hao walidai lazima wakaguliwe kwanza.

“Hivyo mtu anaona kuliko aendelee kusumbuliwa bora awape fedha wamwache aendelee na biashara yake,” alisema Peter.

Kuhusu upatikanaji wa sukari, Peter alisema kuna usumbufu mkubwa wa kuipata bidhaa hiyo hali inayosababisha  iendelee kuuzwa bei ya juu kuliko  iliyoelekezwa na serikali.

“Tunapanga foleni kuanzia asubuhi hadi jioni kutafuta kibali na hatimaye usipate sukari, inabidi tutumie madalali ambao nao wanaongeza gharama ya sukari,” alisema.

Alisema kutokana na usumbufu huo, hadi kuifikisha sukari dukani, mfuko wa kilo 20 unagharimu Sh 39,000 hadi Sh 40,000 badala ya Sh 35,000 ya awali.

“Agizo la serikali ni kwamba hadi kufika kwa walaji inapaswa kuuzwa kwa Sh 1,800, lakini bei hiyo ndiyo tunayouziwa na wakala, hivyo lazima tutauza Sh 2,000 na hadi kumfikia mlaji bei itakuwa kati ya Sh 2,100 na Sh  2,600 kwa kilo,” alisema Peter.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema kinachofanywa na polisi ni kuhimiza wafanyabiashara kutoficha sukari kwa sababu  ni makosa kwa mujibu wa sheria.

Alisema ukaguzi unaofanywa na   polisi ni wa kawaida mtu anapotiliwa shaka na unafanywa kwa  nia njema.

Senso aliwataka wananchi kutoa taarifa kama kuna askari atakayeonyesha nia mbaya ya kutaka kupewa rushwa.

“Askari wanafanya ukaguzi kwa nia njema   wanapotilia shaka mtu na wakimaliza uchunguzi wao kama hakuna ukiukwaji wa taratibu huyo mtu anaachiwa lakini kama wapo askari wenye nia mbaya tunaomba wananchi watoe taarifa,” alisema Senso.

Wakati huo huo, mmiliki wa Kampuni ya Tanzania Commodities Trading Group, Murtaza Dewji amekana kuficha sukari tani 2,990 zilizokutwa Bandari Kavu (ICD) ya PMM iliyopo Vingunguti,  Dar es Salaam.

Sukari hiyo ambayo ilihusishwa moja kwa  moja na Kampuni ya Mohamed Enterprises, ilidaiwa kukamatwa juzi katika msako maalum ulioendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Dewji alikanusha kampuni yake kuwa na uhusiano na Metl, akisisitiza hajawahi kuficha sukari.

Alisema  sukari aliyonayo  iko kwa halali na inavyo vibali vyote stahiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles