25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WADAIWA KUUA, NDUGU WAGOMA KUZIKA

Na Ashura Kazinja – Kilosa

WANANCHI wa Kijiji cha Ruhembe wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, wamegoma kuzika maiti ya Salim Muheka (17), ambaye anadaiwa kuawa na polisi wa Kitengo Maalum.

Kijana huyo anadaiwa kuawa juzi na askari hao akituhumiwa kuwa  mhalifu wa matukio ya Kibiti  mkoani Pwani.

Wananchi wameipa serikali  siku tatu   itoe majibu sahihi kuhusu tukio hilo.

Muheka ambaye amehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Ruaha  mwaka huu, aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na askari hao hali iliyozua taharuki kwa wananchi wa kijiji hicho.

Tukio hilo limevuta hisia kwa wananchi huku Jonsia Kitabu, mkazi wa Ruhembe akisema hawajui sababu za kijana huyo kupigwa risasi mpaka kusababisha kifo chake.

Alisema wananchi  wameamua hawatamzika mpaka wajue sababu.

Baada ya kupata taarifa hiyo,  Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema),  alikwenda nyumbani kwa wazazi wa marehemu huyo na kukuta umati wa wananchi wakilia  huku wakitaka uchunguzi huru kuhusu tukio la kuuawa kijana huyo.

“Ninapenda kusema tukio hili halikubaliki. Nami kama mwakilishi wenu nalia nanyi, tupo pamoja kwa sababu  hatuwezi kuona damu ya wananchi maskini ikiendelea kupotea kwa mauaji kama haya,” alisema Haule.

Baba mzazi wa marehemu, Said Muheka alisema   hawezi kumzika mtoto wake   mpaka apate tamko kwa mauaji yaliyotokea.  Aliiomba serikali kutoa tamko juu ya tukio hilo.

Kauli ya baba mzazi wa mtoto huyo ilizidi kuibua kilio kutoka kwa wananchi waliokuwa wamefurika nyumbani kwake.

Hali hiyo ilimfanya mbunge huyo ashindwe kujizuia naye akabubujikwa na machozi huku akiahidi kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchema, aingilie kati suala hilo kabla ya wananchi hawajajichukulia sheria mkononi.

“Yaani sisi tumekuwa wanyonge, tunakufa kama hivi kwenye mafungu, narudia Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri Mkuu, hawa watu wakiendelea hivi kuna wakati hapa mtu hataweza kufanya kazi tena,” alisema Mbunge huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alithibitisha kuuawa kwa kijana huyo.

Alisema taarifa aliyopewa na kikosi kazi ilieleza kuwa aliyeuawa alikuwa akijihusisha na masuala ya ugaidi na alikuwa akitafutwa.

“Kikosi kazi kinasema huyu kijana alikuwa anajihusisha na masuala ya ugaidi.

“Tumejaribu kufuatilia… kuna wengine tena wanatafutwa maeneo hayohayo kwa matukio ya aiana hiyo,” alisema Kamanda Matei.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles