24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

BANDARI BADO HAKUJATULIA

PATRICIA KIMELEMETA

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameirarua Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Ili kuongeza ufanisi TPA, Serikali inatarajia kupeleka Naibu Mtendaji Mkuu mpya ili kusimamia suala hilo kwa umakini zaidi kutokana na aliyekuwepo kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzuia mpango aliodai wa ‘wajanja’ kutaka kuzitoa bandarini bila kulipa kodi trela 44 kwa kutumia jina lake.

Akizungumza baada ya kufanya ziara bandarini hapo jana, Waziri Mbarawa alisema licha Rais Dk. John Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa kubaini uozo kadhaa, menejimenti pamoja na Bodi hazijafanya juhudi za kurekebisha ‘madudu’ hayo.

Wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza  bandarini hapo na kukuta magari 53 ya kubebea wagonjwa yasiyokuwa na mwenyewe licha ya nyaraka kuonyesha yaliagizwa na ofisi ya rais.

Katika ziara hiyo, Profesa Mbarawa pia alibaini kuwapo makontena zaidi ya 100 ambayo yaliingia nchini tangu mwaka 2011 na 2012 na wahusika wa kontena hizo hawajulikani lakini mpaka sasa bodi haijatoa uamuzi kuhusu suala hilo.

“Nimesikishwa sana na kitendo cha bodi ya wakurugenzi wa TPA kushindwa kufanya uamuzi wowote kuhusiana na magari 53 yasiyokuwa na wenyewe, trela 44 zilizotaka kutoka bila ya kulipiwa ushuru na leo nimekuta makontena 100 ambayo mmiliki wake hajulikani.

“Sasa nashindwa kuelewa sababu za kasoro hizi kufumbiwa macho wakati mnaziona, nimesikitishwa sana na utendaji wenu.

“Tunaleta naibu mtendaji mkuu ambaye atasimamia operesheni, naomba apewe ushirikiano ili kusaidia Serikali huyu ambaye anakaimu tunamuondoa ameshindwa kwenda na kasi yetu,” alisema Prof. Mbawara.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Ignas Rugaratuka alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanaitendea haki nafasi waliyopewa kwa kusimamia mabadiliko ndani ya bandari.

MTANZANIA limepata taarifa kwamba nafasi aliyetajwa kuondolewa na Profesa Mbarawa ni Kaimu Naibu Mkurugenzi mkuu, Utekelezaji bandarini hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema tangu aingie katika mamlaka hiyo wamekuwa wakifanya jitihada za kurekebisha upungufu na kumuahidi waziri kuwa ataongeza jitihada zaidi.

“Kama ni mabadiliko tumefanya makubwa sana hasa katika utawala na uongozi ila kila anayehusika katika sekta hiyo anapaswa kutoa msaada,” alisema Mhandisi Kakoko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles