29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI: NABII TITO ANA MATATIZO YA AKILI

RAMADHAN HASSAN na TAUSI SALUM-DODOMA


JESHI la Polisi mkoani Dodoma limesema Tito Machibya, maarufu kwa jina la Nabii Tito (44) ni mgonjwa wa akili baada ya kupimwa katika Hospitali ya magonjwa ya akili ya Mirembe.

Taarifa ya polisi imetolewa wakati kukiwa na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Machibya akicheza muziki pamoja na wanawake wawili huku  akiwa amevaa mavazi yanayofanana na ya kichungaji yenye nembo ya msalaba.

Akizungumza jana Mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema Machibya alifanyiwa uchunguzi wa afya ya akili Dk. Dickson Philipo wa Hospitali ya Mirembe na kugundulika kuwa ni mgonjwa wa akili kwa muda mrefu.

Kamanda Muroto alisema Machibya aliwahi kufanyiwa uchunguzi  Juni 6, 2014 katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili (MNH)na kugundulika kuwa na ugonjwa wa akili.

Alisema alitibiwa ugonjwa huo na kuruhusiwa kurejea nyumbani na Daktari wake aliyetambulika kwa jina moja la  Dk.William huku akitakiwa kurudi tena kwa uangalizi wa tiba Julai 9, 2014 lakini hakurejea.

“Baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa anaonekana Dodoma akifanya vitendo vya udhalilishaji na upotoshaji kwa jamii ndipo tulimkamata na kumpeleka katika Hospitali ya Mirembe kwa uchunguzi zaidi.

“Baada ya uchunguzi uliofanywa na Dk. Dickson Philipo wa hospitali hiyo amegundulika kuwa ni mgonjwa wa akili kwa muda mrefu,” alisema Kamanda Muroto.

Aidha, alisema jambo la kushangaza pamoja na kuwa na hali hiyo lakini ameendelea kuhamasisha maovu ambayo ni kinyume na  desturi za Watanzania huku akionekana ni mtu mwenye akili timamu.

“Lakini cha kushangaza pia kuna watu wanamshabikia na kuambatana naye, Jeshi la Polisi litawachukulia hatua kali watu hao kwani ni kinyume na utamaduni ya Tanzania,” alisema

Kamanda Muroto alisema polisi wanaendelea kumshikilia kwa upelelezi zaidi na kunusuru maisha yake.

“Tunamshilia kwanza, kabisa tunanusuru maisha yake kwa kuwa watu wenye dini hii wanaweza wakaona wanadhalilishwa hivyo wanaweza  kumdhuru, pili anaonekana ni mgonjwa wa akili lakini anafanya makosa ya kijinai hivyo tunamfanyia upelelezi zaidi,” alisema kamanda huyo.

KAULI YA NABII TITO

Akiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma, Nabii Tito alisema mambo yote anayoyazungumza na kuyafanya anayotoa katika biblia.

“Mnataka nini? kwani leo unabii unaenda kukamilika haya ninayoyazungumza ninayatoa katika kitabu cha Biblia, Mungu mwenyewe ananionyesha kichwani, ndiyo ninayoyafanya,” alisema.

Machibya alisema yeye kama Nabii hakuna kinachomtatiza kufanya kama ilivyo kwa watu wengine.

Alisema waumini wake lazima wawe na umbo na sura nzuri kwa sababu anahitaji kuwa na watu wa aina hiyo ambao nao watasadiki kile anachokizungumza yeye.
Machibya aliwaambia polisi kuwa yupo mbioni kumtafuta msanii maarufu nchini, Wema Sepetu kwa sababu ana imani atashawishi watu wengi kuingia katika kanisa lake analoliabudu.

Kuhusu unywaji wa pombe kanisani alisema si tatizo kwa sababu waumini wake wakiingia kanisani huwapa ili wanywe vizuri.

“Katika Kanisa letu kunywa pombe ni ruhusa na ukitoa Sh 12,000 kama sadaka unapata bia tano na kama  hujalewa tunakurudishia fedha yako,”alisema.

UMKD WALAANI

Katibu wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma,(UMKD) Askofu Dk Eliya Mauza alisema Umoja huo hauwezi kukubali udhalilishaji unaofanywa na Machibya na alitoa wito kwa polisi kumchukulia hatua kali zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles