NA BENJAMIN MASESE, MWANZA
ASKARI wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, PC Joel Francis (41) mwenye namba F.4965 anadaiwa kumpiga Donald Magalata (30) kwa fimbo na kumsababishia kifo.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni wiki moja imepita,baada ya askari mwingine mkoani hapa Dau Elisha mwenye namba H 852 PC wa kituo cha Nyamagana kumuua askari mwenzake PC Petro Matiko wenye namba H 5950 kwa risasi na baadaye kujipiga risasi kichwani na kufariki dunia papo hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema tukio hilo lilitokea Januari mosi, mwaka huu saa moja asubuhi katika kambi ya Polisi Mabatini.
Alisema siku hiyo, PC Francis alikwenda nyumbani kwake na kumkuta marehemu ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu akiwa amelala.
Alisema baada ya askari huyo kuingia ndani kwake, aligundua pochi yake ya kutunzia fedha, kadi mbili za benki na kitambulisho cha kazi vyote vilikuwa havionekani ndipo alipoanza kuhoji.
“Marehemu alikuwa rafiki yake PC Francis, alikuwa akimsaidia kazi mbalimbali za nyumbani, ingawa marehemu alikuwa akifanya kazi ya ulinzi hotel ya Mwanza iliyopo katikati ya jiji.
“Sasa mzozo huo, ulisababisha PC Francis kumfunga pingu miguuni marehemu na kuanza kumpiga ovyo sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia fimbo kitendo kilichosababisha kupiga kelele kuomba msaada.
“Kelele za kuomba msaada ziliwafanya majirani zake pale kambini wafike na kumkuta akiwa na hali mbaya na kumchukua hadi Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili matibabu,”alisema.
Alisema kutokana na kipigo alichopata, marehemu alifariki Januari 2, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu.
Alisema tayari jeshi hilo, linamshikilia Pc Francis kwa mahojiano juu ya tukio hilo na atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa taratibu wa kijeshi.
Kamanda Kamugisha, alisema anashangazwa na tukio hilo kufanywa na askari ambaye anapaswa kusimamia sheria na haki za binadamu, huku akisisitiza kitendo hicho kisichukuliwa kama maadili na maagizo ya jeshi la polisi, bali ni tabia ya mtu mmoja.