NA AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini bunduki gani iliyopiga risasi na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa Februari 17, mwaka huu akiwa katika daladala eneo la Kinondoni Studio baada ya risasi inayodhaniwa kupigwa na polisi waliowatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokuwa wakiandamana kuelekea katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni zilizopo Magomeni na baada ya tukio hilo kutokea, Mambosasa alitangaza kuwashikilia askari sita kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumzia maendeleo ya uchunguzi huo ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mambosasa, alisema upelelezi bado unaendelea ili kuweza kumbaini askari aliyetenda tukio hilo.
“Ikumbukwe silaha moja ambayo haijajulikana ni ipi ndiyo imeenda ikamgusa Akwilina, lakini askari wale kama ulivyojua walikuwa ni wengi pia kulikuwa hakuna ushahidi kwamba ni yupi alikuwa ametenda kosa hilo hivyo upelelezi bado unaendelea, tutakapokuwa tumekamilisha upelelezi tutakuja katika vyombo na kuwaeleza nini kinaendelea.
“Kama mnakumbuka polisi walipokamatwa tulieleza bayana kwamba upelelezi unafanyika ili kujua ni nani ametenda kosa lile,” alisema.
Mambosasa alisema suala la upelelezi linaendelea kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa ili kumbaini aliyetenda kosa hilo.
Licha ya kutoa ufafanuzi huo, lakini awali Mambosasa alionekana kuchukizwa jambo lililosababisha kuanza kumshambulia mwandishi wa gazeti hili aliyeuliza swali hilo kwa kumtuhumu kuwa ni mfanyakazi wa Chadema.
Kauli hiyo aliitoa baada ya kutakiwa kutoa taarifa ya uchunguzi wa askari sita walioshikiliwa baada ya kutajwa kudaiwa kuhusika na kifo cha Akwilina kwa kuwa baadhi ya viongozi wa Chadema wameshafikishwa mahakamani kwa madai ya kuhusika na maandamano hayo.
“Kwanza ninachotaka nitofautiane na wewe, najua unafanyia kazi Chadema lakini mimi ninachokijua wale ni watuhumiwa na tunachoweza kusema sisi ni kwamba watuhumiwa wale walipelekwa mahakamani si watu wa Chadema.
“Chadema haipelekwi mahakamani, matendo ya mtu ndiyo yanamfanya apelekwe mahakamani kwa hiyo wale walipelekwa mahakamani kutokana na yale waliyokuwa wanayafanya,” alisema.