30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi anayetuhumiwa kushiriki udanganyifu mitihani kidato cha nne kufikishwa mahakamani kesho

*18 wengine tayari wamefikishwa mahakamani

Ramadhani Libenanga, Morogoro

SIKU chache baada ya Baraza la Mitihani (Necta) kutangaza kuwachukulia hatua waliojihusisha na udanganyifu katika mitihani ya  Taifa ya kidato cha nne iliyofanyika  mwaka jana,  tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia askari polisi mwenye namba G.7381   PC Hamisi  wa kituo cha polisi wilaya ya Malinyi kwa tuhuma hizo.

Askari huyo anadaiwa kufanya kosa hilo katika shule ya sekondari Tumaini Lutheran Seminary  iliyopo wilaya ya Malinyi Morogoro ambayo imefutiwa matokeo  na Necta wakati akisimamia ulinzi na usalama wa mitihani hiyo.

 Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wilbrod Mutafungwa alisema  baada ya kupata taarifa hizo  jeshi hilo lilifanya uchunguzi   kwa sasa askari huyo tayari ameshafunguliwa mashtaka ya kijeshi kwa kukiuka maadili mema ya Jeshi la Polisi.

“Utaratibu wa mashitaka ya kijeshi  utakapokamilika hatua stahiki kwa mujibu wa miongozo,kanuni na taratibu za jeshi la polisi zitachukuliwa,”alisema Mutafungwa.

Aidha Mutafungwa alipozungumza tena na gazeti hili baadae alisema kuwa tayari maandalizi ya kumpeleka mahakamani yameshafanyika   na kwamba mshitakiwa huyo anatarajiwa kupandishwa  katika mahakama ya wilaya ya Malinyi kesho.

Alipoulizwa endapo Mkuu wa shule hiyo ni miongoni wa watuhumiwa watakaunganishwa na askari huyo  ili aweze kufikishwa mahamakani alimtaka mwandishi  kusubiri  jibu hilo  la swali hilo kesho atakapofika  mahakamani.

Aidha Mutafungwa alisema kuwa tayari watuhumiwa 18 wakiwemo wasimamizi,walimu, na wanafunzi wameshafikishwa  mahakamani  kwa makosa mbalimbali  yanayohusu udanganyifu wa mitihani hiyo.

Alhamisi ya wiki hii Katibu Mtendaji Necta Dk. Charles Msonde alipokuwa akitangaza matokeo ya mtihani huo jijini Dodoma, alisimulia jinsi uongozi wa shule ya Sekondari Tumaini Lutheran Seminary ilivyofanya udanganyifu kwenye mtihani wa kidato cha nne ambapo walimu na askari walishiriki.

Alisema walimu sita na wanafunzi wa kidato cha pili na tatu, pamoja na askari aliyekuwa anasimamia mitihani hiyo, alishiriki udanganyifu kwa kutoa maswali kwenye chumba cha mtihani na kuingiza majibu kwenye chumba hicho.

Alisema kutokana na udanganifu huo, baraza limefuta matokeo ya wanafunzi wote wa shule hiyo.

Alisema Necta  kwa kushirkiana na kamati ya mitihani ya Wilaya ya Malinyi na ile ya Mkoa wa Morogoro, walifika shuleni hapo na kubaini uongozi wa shule kwa kushirikiana na walimu sita, watahaniwa na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu na pili na askari walipanga njama ya udanganyifu wa mitihani.

ILIVYOIBIWA

Dk.Msonde alisema uongozi wa shule uliwapatia jukumu maalum baadhi ya wanafunzi wa kidato cha pili na cha tatu kuchukua mitihani kutoka kwa watahiniwa kupitia kwenye madirisha na matundu yaliyotobolewa.

Alisema matundu hayo yalikuwa yametobolewa kwenye vyumba vya mitihani na kuwafikishia walimu walimu wa masomo husika waliokuwa wamewekwa kwenye chumba maalum kwa lengo la kuwatolea majawabu.

“Wanafunzi hao walishirikiana na walimu hao kunakili majibu yaliyoandaliwa na hatimaye kwa kushirikiana na askari polisi aliyekuwa kituoni,majawabu yalirejeshwa kwa watahiniwa kwenye chumba cha mtihani,”alisema Dk.Msonde.

Alisema Kamati ilibaini uwepo wa karatasi nyingi zilizokuwa na majibu ya somo la Kemia nje ya vyumba vya mitihani ambazo zilifanana na maswali yote ya mtihani wa somo hilo ambao ulikuwa ukiendelea kufanyika.

Katibu huyo alisema walimu wote walioshiriki hujuma hiyo walikamatwa,kuhojiwa na kukiri kuhusika kwao kufanya udanganyifu katika mitihani ya masomo ya Hisabati ,Jiografia, Historia na Kemia

Alisema maamuzi ya Baraza hilo ni kufuta matokeo yote ya watahiniwa 57 wa shule hiyo.

“Pia kuifungia shule ya Sekondari S0983 Tumaini Lutheran Seminary kuwa kituo cha mitihani hadi Baraza litakapojiridhisha kuwa kituo hicho ni salama kuendesha mitihani ya taifa,”alisema.

Aidha aliagiza Bodi ya shule hiyo iwachukulie hatua kali za kinidhamu wanafunzi wa kidato cha pili na cha tatu walioshiriki kufanikisha udanganyifu huo.

Aidha aliagiza  mamlaka husika iwachukulie hatua stahiki walimu na askari Polisi walioshiriki udanganyifu kwa mujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles