Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM |
KOCHA Mkuu wa Singida United, Hans van der Pluijm, amesema hawezi kuwapa presha wachezaji wake kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba.
Singida United itakuwa nyumbani kuikabili Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Mei 13, Uwanja wa Namfua, mkoani Singida.
Singida United katika mchezo wake uliopita ikiwa nyumbani, ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji.
Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, Singida United inashika nafasi ya tano, ikiwa na pointi 41 sawa na Tanzania Prisons inayotofautiana nayo kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm, alisema anaamini kila mchezaji wa timu hiyo anatambua majukumu yake awapo uwanjani, hivyo haoni sababu ya kuwapa presha ya kile wanachotakiwa kukifanya.
“Mchezo wa raundi ya kwanza tulipokutana na Simba tulipoteza kwa kufungwa mabao 4-0, hata hivyo kulikuwa na mazingira yaliyotufanya tupoteze lakini kwa sasa tutahakikisha haturudii makosa kwa mara nyingine na tunachoangalia ni pointi tatu,” alisema.
Alisema kwa sasa anayafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita, lengo likiwa ni kuvuna pointi zote tisa katika michezo yao mitatu iliyosalia.