30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm awasha moto

pluijm*Awajia juu mastraika wake, Ngoma arejea kuiua African Sports

HASSAN BUMBULI NA OSCAR ASSENGA, TANGA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kurejea kwa mshambuliaji Donald Ngoma kutaongeza matumaini ya ushindi kwa kuwa nyota huyo ana uwezo wa kufiti kwenye kombinesheni mbili muhimu alizoziunda.

Kurejea na straika huyo Mzimbabwe ambaye ni mkali wa kupachika mabao  kunaweza kumaliza tatizo la ubutu wa safu ya ushambuliaji iliyoonekana juzi katika mechi dhidi ya Mgambo Shooting ambayo ilimalizika kwa matokeo ya suluhu.

Akizungumza na gazeti jana, Pluim alisema kukosekana kwa Ngoma aliyekuwa majeruhi kumechangia kuvurugika kwa mfumo wake kwa kuwa wachezaji wengine bado hawajaelewana vizuri.

“Tumejenga mifumo miwili ambayo ngoma ni mtu muhimu kwa kuwa ana uwezo wa kufiti, mifumo mingine ipo lakini bado washambuliaji wengine hawajaelewana vizuri, hivyo kuna ulazima wa kulifanyia kazi jambo hili haraka iwezekanavyo,” alisema.

Kwenye kikosi cha Yanga Pluijm ametengeneza kombinesheni ya Ngoma, Amissi Tambwe na Simon Msuva lakini katika kombinesheni nyingine amemuondoa Msuva na kumuongeza Malimi Busungu.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, alichoshwa na makosa ya kizembe yaliyofanywa na washambuliaji wake juzi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mgambo Shooting hali iliyomfanya awajie juu nyota hao waliokosa mabao mengi.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, safu ya ushambuliaji ya Yanga iliyoongozwa na Tambwe, Busungu na Msuva ilipoteza nafasi zaidi ya 16 za kufunga mabao na kusababisha kukosa pointi tatu muhimu.

Kutokana na hali hiyo, Pluijm alisema ni lazima washambuliaji hao warudi kusoma jinsi ya kulenga lango kwani haiwezekani kutengeneza nafasi nyingi na kupoteza zote jambo ambalo alianza kulifanyia kazi kwenye mazoezi ya jana.

“Si kwamba nawalaumu washambuliaji wangu, lakini lazima watalipia nafasi walikozosa na kutugharimu kukosa pointi tatu kwa kufanya mazeoezi ya ziada, na sitakuwa na mchezo katika kutekeleza jambo hili,” alisema.

Naye daktari wa timu hiyo, Harun Alluy, aliwatoa hofu mashabiki wa Yanga akidai kuwa Ngoma aliyekuwa akimalizia dozi yake ya matibabu, keshokutwa atakuwa fiti kuongoza mashambulizi dhidi ya African Sports.

“Ngoma alikuwa akisumbuliwa na mkono ambao ulihama kwenye njia yake ambapo alipata matibabu na tumeurudisha katika hali yake ya kawaida na keshokutwa atarejea uwanjani,” alisema.

Kauli ya daktari huyo inaweza kurejesha matumaini kwa mashabiki wa Yanga kutokana na wasiwasi waliopata baada ya washambuliaji wengine wa timu hiyo kukosa mabao mengi ya wazi katika mchezo  uliopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles