26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm atuliza mashabiki wanaomlilia Ngoma

Hans-van-der-PluijmNA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo akidai ametengeneza kikosi imara kinachoweza kupata ushindi kutokana na ushirikiano uwanjani na si kwa kutegemea mchezaji mmoja mmoja.

Mashabiki wa Yanga juzi waliingiwa na wasiwasi wa kukosa ushindi baada ya kukosekana uwanjani kwa mshambuliaji hatari Mzimbabwe Donald Ngoma na Thabani Kamusoko katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola.

Nyota hao walikosekana kwenye mchezo wa juzi uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na kukabiliwa na adhabu ya kadi za njano walizopata katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Licha ya kikosi cha Wanajangwani hao kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani, pia wachezaji walikosa nafasi nyingi za kufunga walizotengeneza hali iliyoibua maswali mengi kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia pambano hilo ambao walikuwa wakimkumbuka Ngoma.

Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya mchezo huo, Pluijm alikiri kuwa wachezaji  walipoteza nafasi nyingi na kukosa mabao kipindi cha kwanza lakini walionyesha umakini kipindi cha pili ambao ulisaidia kupatikana matokeo ya ushindi.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema matokeo mazuri yametokana na ushirikiano wa timu nzima na siku zote huwa hafikirii ushindi kutokana na mchezaji mmoja, hivyo mashabiki wanatakiwa kuondoa dhana kwamba baadhi ya wachezaji wakikosekana ushindi ni vigumu kupatikana.

“Pamoja na kuchelewa kupata mabao wachezaji walicheza kwa kujituma ili tuweze kupata ushindi muhimu ingawa haukuwa mnono, hata hivyo hatuwezi kubweteka kwani bado tuna kazi ngumu ya kucheza mechi ya marudiano ugenini,” alisema Pluijm.

Pluijm alisema mchezo wa ugenini utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa, hivyo ni lazima wazidishe umakini na kuhakikisha wanatumia vyema nafasi watakazopata ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wake kocha mkuu wa timu ya Sagrada Esperanca, Zoram Manojlovec, alikiri kuwa watakuwa na kazi ngumu ya kuifunga Yanga nyumbani watakaporudiana Mei 17, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga, Manojlovec alisema hali hiyo inatokana na wapinzani wao kuwa imara zaidi pamoja na umakini walioonyesha katika mchezo wa juzi.

“Nilifanikiwa kuwaona Yanga katika mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri kabla ya kukutana nao, leo (juzi) pia wamecheza soka la kuvutia na kutufunga kwani waliwadhibiti vilivyo wachezaji wangu,” alisema.

Alisema bao la pili la Yanga lilifungwa katika mazingira ambayo hawakutegemea kwani lilikuwa la kushtukiza hivyo kuwaondoa wachezaji mchezoni.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles