27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Pluijm aisukia mipango Al Ahly

Hans-Van-De-PluijmNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, amesema sasa wanajipanga upya kabla ya kuvaana na wapinzani wao, Al Ahly ya Misri katika hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika ili kulipiza kisasi cha kuondoshwa nje ya michuano hiyo mwaka 2014.

Yanga imefanikiwa kusonga mbele baada ya kuitupa nje ya michuano hiyo APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 ikiwa ni ushindi wa 2-1 ugenini na sare ya 1-1 nyumbani.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Pluijm alisema licha ya kufanikiwa kusonga mbele wachezaji wake walicheza chini ya kiwango ukilinganisha na uwezo walioonesha katika mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, Rwanda na kushinda mabao 2-1.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema hakufurahishwa na kiwango kilichooneshwa kwani wachezaji hawakuwa na mawasiliano mazuri uwanjani jambo ambalo anahitaji kulifanyia kazi mapema na kujipanga kwa mchezo unaofuata.

“APR walitawala mchezo kwa kiasi kikubwa, waliweza kuonesha utaalamu wao kutokana na kiwango chao, pia walionesha wazi kuwa wanahitaji ushindi kwa kuwa na mawasiliano mazuri uwanjani hali iliyochangia mchezo kuwa mgumu kwa upande wetu.

“Nafurahi tumeshinda ingawa wachezaji hawakuwa na mawasiliano mazuri uwanjani, kwani walionesha kiwango tofauti na tulivyocheza ugenini, marekebisho makubwa yanahitajika kwani haya ni mashindano makubwa yanayohitaji kiwango cha juu,” alisema.

Hata hivyo, Pluijm alisema anawafahamu vizuri Al Ahly kwa kuwa alishawahi kukutana nao na kusoma vizuri mbinu wanazotumia na aina ya uchezaji, huku akidai wanachohitaji sasa ni kujipanga zaidi.

Kwa mara ya mwisho Wanajangwani hao walikutana na Al Ahly Machi 8, mwaka 2014 jijini Alexandria, Misri kwenye mechi ya marudiano na kufungwa bao 1-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1 baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Al Ahly walifanikiwa kuiondosha kwenye michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Kwa upande wake kocha wa timu ya APR, Nizar Khanfir, alimsifia straika wa Yanga, Donald Ngoma, kutokana na kiwango alichoonesha huku akidai ndiye mchezaji aliyewasumbua zaidi.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Zimbabwe, alitibua mipango ya APR waliokuwa mbele kwa bao moja lililofungwa na Faustino Nkinzingabo dakika ya nne, baada ya kuisawazishia timu yake bao dakika ya 28.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles