KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm ameanza kuchonga kutokana na ushindi waliopata dhidi ya African Sports juzi ambapo amesema umesaidia kuwapa nguvu ya kuendeleza kasi yao katika mechi zinazofuata na kuendelea kubaki kileleni.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, juzi waliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya African Sports katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Bao la pekee lililofungwa dakika za lala salama na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, liliiwezesha Yanga kurejea kileleni kwa kufikisha pointi 27 na kuwashusha wapinzani wao Azam FC hadi nafasi ya pili wakiwa wamejikusanyia pointi 26.
Akizungumza na MTANZANIA juzi mara baada ya mchezo, Pluijm alisema licha ya kupata ushindi bado wana kazi kubwa ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza kabla ya kukutana na Stand United ya Shinyanga kesho katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alikiri kuwa mchezo ulikuwa na upinzani mkubwa kutokana na wapinzani wao kucheza kwa umakini mkubwa hali iliyowapa wakati mgumu kupata bao la mapema.
“Pointi tulizopata dhidi ya African Sports zimetupa faraja kubwa hasa kwa kuzingatia mechi iliyopita tuliambulia suluhu dhidi ya Mgambo Shooting, hivyo tunataka kutumia nguvu hii ya ushindi kuendeleza vipigo katika michezo inayofuata,” alisema.
Yanga inahitaji ushindi itakapovaana na Stand kesho ili iweze kuendelea kutamba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, kwani ikishinda itafikisha pointi 30 huku wapinzani wao Azam wakitarajiwa kufikisha pointi 29 kama wataifunga Majimaji keshokutwa.
Yanga ambao wamepania kutetea taji la ubingwa msimu huu, waliingia uwanjani wakiwa wamekamilika kila idara hasa baada ya kurejea dimbani kwa mshambuliaji wao hatari Mzimbabwe, Donald Ngoma ambaye aliikosa mechi dhidi ya Mgambo.
Mashabiki wa African Sports waliokuwa upande wa jukwaa lao walianzisha vurugu zilizosababisha baadhi yao kurushiana viti baada ya kumalizika kwa mchezo lakini zilizimwa na polisi waliokuwepo uwanjani.