22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kerr aumiza kichwa, Tegete historia itajirudia

kerr kazini simba 34MWALI IBRAHIM, DAR NA JOHN MADUHU, MWANZA

WAKATI kocha mkuu wa Simba, Dylan Kerr  akiumiza kichwa kusubiri dakika 90 ziamue mshindi dhidi ya Toto African kesho, kocha John Tegete amejibu mapigo na kudai historia itajirudia kwani lazima wawasambaratishe wapinzani wao.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambapo Kerr ameshindwa kutabiri matokeo ya pambano hilo huku mpinzani wake akijinadi ushindi ni lazima kwa upande wao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kerr alikiri kuwa mechi za ugenini ni ngumu kwao ingawa waliweza kuibuka na ushindi katika Uwanja wa Mkwakani, Tanga huku akieleza kuwa amepanga kufanya mabadiliko kulingana na hali ya uwanja.

“Nimewapa wachezaji wangu mazoezi ya kutosha kama tunavyofanya maandalizi ya kukutana na timu nyingine za Ligi Kuu ili kuhakikisha tunafanya vizuri, hakika hakuna timu ambayo ni rahisi kuifunga hivyo mashabiki wasubiri dakika 90 za mchezo,” alisema.

Mwingereza huyo alisema wachezaji wapo fiti kwa mchezo wa kesho na kikosi tayari kimewasili jijini Mwanza kujiandaa na pambano hilo.

Naye kocha Tegete wa Toto, alisema wamejiandaa kikamilifu kuwashikisha adabu Simba kwa kuwa hawana kikosi imara kinachoweza kumtisha na kutibua mipango yake ya kuondoka na pointi tatu.

 

Alisema baada ya kuisambaratisha Majimaji FC katika mchezo uliopita, sasa wamehamishia nguvu katika pambano dhidi ya Simba ambapo amedai kikosi kipo fiti na wachezaji wameimarika kwa kiwango cha hali ya juu.

 

“Tumejiandaa vya kutosha kuikabili Simba ambayo ni timu ya kawaida, wachezaji wana ari kubwa ya ushindi hivyo historia ni lazima ijirudie kwani tumekuwa tukiwafunga nyumbani na ugenini, wajiandae kwa matokeo mabaya,” alisema.

 

Toto ambayo ilishiriki michuano ya Ligi Kuu kwa mara ya mwisho msimu wa 2012/13, kabla ya kushuka daraja iliichapa Simba bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 waliporudiana Uwanja wa CCM Kirumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles