KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, amesema leo kikosi chake kitaanza maandalizi rasmi ya kujiweka fiti kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR ya Rwanda utakaofanyika Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ikicheza ugenini Yanga ilifanikiwa kuwachapa wenyeji wao APR mabao 2-1 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa Uwanja wa Amahoro, mjini Kigali, Rwanda.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema timu hiyo inakabiliwa na mchezo mgumu wa marudiano dhidi ya wapinzani wao, hivyo akili yake ameielekeza kwenye kwenye maandalizi ya pambano hilo.
“Licha ya kupata ushindi ugenini, bado kuna makosa niliyobaini kwa wachezaji ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka kabla ya kurudiana Jumamosi hapa nyumbani,” alisema.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema kwa sasa hawezi kuzungumza jambo lolote kuhusu Ligi Kuu hadi watakapomalizana na APR kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika michuano hiyo.