BEKI wa Barcelona, Gerard Pique, amesema klabu hiyo bila ya mshambuliaji wake, Lionel Messi, haiwezi kufika kokote.
Barcelona juzi ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Sevilla katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania, ambapo kwa sasa klabu hiyo inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi na wapinzani wao Real Madrid ikishika nafasi ya nne.
Messi kwa sasa ni majeruhi ambapo atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili hivyo kwa sasa klabu hiyo imeanza kuyumba kutokana na kumkosa nyota huyo.
Pique amesema klabu hiyo katika kipindi hiki ina wakati mgumu kwa kuwa inamkosa mshambuliaji huyo.
“Tulitarajia kuanza vizuri msimu huu kwa ajili ya kutetea ubingwa wetu, lakini hali imekuwa tofauti na wakati mgumu kutokana na kumkosa mshambuliaji wetu, Lionel Messi ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa wiki saba mpaka nane kwa mujibu wa daktari.
“Ninaamini mchezo wa juzi tumepoteza kutokana na kumkosa Messi na Iniesta ambaye naye ni mgonjwa, lakini sio sababu kwa kuwa hata Sevilla walikuwa na wachezaji wao ambao ni wagonjwa.
“Kikubwa ni kwamba hatukuwa na bahati maana tumekosa bahati, baadhi ya michezo ambayo tumeipoteza tulishindwa kuzitumia nafasi vizuri,” alisema Pique.