NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema muswada wa sheria mpya ya takwimu umefuata makubaliano ya nchi za Afrika na duniani kuhusu utengenezaji na usambazaji wa takwimu.
Pinda aliyasema hayo jana mara baada ya kufungua kongamano lililolenga kutoa elimu kwa wakuu wa ofisi za takwimu wa nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza juu ya uongozi na usimamizi.
Alisema lengo la sheria hiyo ambayo inasubiri kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete ili kuanza kutumika, ni kutekeleza makubaliano ambayo yanazitaka nchi za Afrika kuhakikisha masuala ya takwimu yanabaki kwa mamlaka husika badala ya kufanywa na kila mtu.
“Ni makubaliano ya Afrika na dunia kwa ujumla kwamba ni vizuri masuala yanayohusu takwimu yasimamiwe na vyombo husika,” alisema Pinda na kuongeza kuwa takwimu zinatakiwa zitolewe kwa usahihi.
“Hata Serikali inaweza kuadhibiwa kwa kutoa takwimu zisizo sahihi,” aliongeza.
Alifafanua kuwa usahihi wa takwimu unahitajika kwa sababu zina madhara katika utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo, hivyo kupotosha kunaweza kuharibu mipango hiyo.
Awali akifungua kongamano hilo, Pinda alizitaka taasisi za kimataifa kutoa taarifa za takwimu zenye manufaa kwa maendeleo ya Waafrika na pia ziwe katika lugha rahisi inayoeleweka na viongozi wa kisiasa na zitolewe katika njia rahisi kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia.