26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wakuu wa nchi za Kusini mwa Afrika kumzika Mbita

mbitaChristina Gauluhanga na Adam Mkwepu, Dar es Salaam
WAKATI nchi nne za kusini mwa Afrika zikithibitisha kushiriki kwenye mazishi ya Brigedia Jenerali Hashim Mbita (82) yatakayofanyika kesho katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, baadhi ya marafiki waliomfahamu marehemu kwa miaka mingi wamesema ameacha pigo na mchango wake unatambuliwa na mataifa mbalimbali.
Mtoto wa marehemu, Idd Mbita, alisema nchi za Zimbabwe, Namibia, Msumbiji na Angola zimethibitisha kutuma wawakilishi katika mazishi ya baba yao.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti nyumbani kwa marehemu Chang’ombe Madukani jijini Dar es Salaam, baadhi ya wasomi pamoja na watu maarufu walimzungumzia Mbita kama mtu pekee na mpigania uhuru wa kweli katika nchi za Kusini mwa Afrika.
Profesa Issa Shivji alisema kuwa kuondoka kwa mkongwe huyo ni pigo la kitaifa kwani alikuwa mwakilishi mzuri wa kizazi cha kizalendo kilichopita.
“Taifa linatakiwa lijitafakari kwa umakini kwani bado kazi ya ukombozi haijakamilika na hivi sasa Afrika hakuna kiongozi yeyote anazungumzia ukombozi wakati bado tunatawaliwa na wakoloni kiuchumi. Aliyethubutu kulizungumzia ni Rais wa Guenea Bissau, Amil Carcabiral pekee ambaye ndie anaonekana kupambana dhidi ya hali hiyo.
“Unajua Mbita alikuwa katika kamati ya ukombozi enzi za Mwalimu Nyerere na yeye ni mwakilishi mzuri wa kizazi cha kizalendo cha wakati huo na ataendelea kukumbukwa kwa kazi aliyoifanya,” alisema Shivji.
Mwanafunzi aliyesoma naye kidato cha nne, Khalid Mtwangi, alisema alimfahamu Mbita tangu miaka ya 1950 wakiwa katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora (Tabora Boys) na baada ya kumaliza kila mtu alienda kuhangaika na maisha ingawa waliendeleza mawasiliano ya karibu.
Baadhi ya viongozi waliofika nyumbani kwa marehemu kuhani msiba ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na wastaafu mbalimbali.
Shughuli za kuaga mwili wa marehemu zitafanyika katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi Lugalo na kisha mwili utarudishwa nyumbani kwake kabla ya kupelekwa kuswaliwa katika Msikiti wa Mtoro na baadaye mazishi yatafanyika katika makaburi ya Kisutu.
Marehemu Mbita ameacha watoto sita na wajukuu tisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles