NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
RAIS Jakaya Kikwete ameonyesha kuhofia nguvu ya upinzani, baada ya kudai picha zinazotolewa na vyombo mbalimbali vya habari zikionyesha mahudhurio makubwa ya wananchi katika mikutano ya hadhara ya mgombea wa urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa si halisi.
Licha ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutomtaja moja kwa moja Lowassa, alidai picha za mgombea huyo ambazo zinaonyesha umati mkubwa uliojitokeza wakati wa uchukuaji fomu ya kuwania urais kwenye Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mikutano ya hadhara katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya zimeunganishwa kwa kompyuta.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam jana katika mkutano uliojaa vijana wengi wa CCM, Rais Kikwete alisema picha hizo zimeunganishwa kwa kompyuta, hivyo basi hawawezi kutishika nazo kwa sababu mgombea wao, Dk. John Magufuli anatosha.
“Msitishike na picha zinazoonyeshwa kwenye mitandao kwa sababu zimeunganishwa kwa kompyuta, mgombea wetu anatosha, mnapaswa kujiamini na kuamini kuwa Oktoba 25, mwaka huu tutashinda kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete, alitumia hotuba yake kumsifia Dk. Magufuli kuwa ni mchapakazi, mwaminifu, mwadilifu na mbunifu, na kwamba matatizo yanayojitokeza katika maeneo yake anaweza kuyatatua mwenyewe bila ya kushirikisha viongozi wengine, hivyo wananchi wanapaswa kumuunga mkono ili aweze kupata ushindi.
Alisema viongozi wazembe, wababaishaji, walarushwa na wasiopenda maendeleo wanamchukia kutokana na tabia zao, na kwamba siku zote huwa hakubali kushindwa jambo.
“Walarushwa, wababaishaji, wazembe na wale wasiopenda maendeleo watamchukia Dk. Magufuli kwa sababu wanamjua nini anachokitaka ili wananchi waweze kupata maendeleo,” alisema.
Alisema mgombea huyo, ni sampuli nyingine kwani tofauti na marais waliopita, yeye aliweza kumchagua mwanamke kuwa mgombea mwenza bila ya kuwa na wapambane wala mbwembwe.
Kikwete alisema kutokana na hali hiyo, Dk. Magufuli hana makuu, jambo ambalo limemfanya kuendesha shughuli zake kimya kimya.
Akitoa mfano, alisema wakati yeye anagombea urais mwaka 2005, wapambe walikuwa wakimuunga mkono japo hawakuwa na mbwembwe nyingi.
Alisema chama hicho, kimeamua kumchagua kiongozi huyo kwa sababu ni mtu anayependa kuona maendeleo kwa yale anayoyafanya na yale anayopewa kuyafanya, hivyo wanaamini atawatumikia wananchi ili waweze kupata maendeleo.
Naye Dk. Magufuli aliwataka wana CCM wawe wamoja na wafanye kampeni nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, kitanda kwa kitanda, shuka kwa shuka na uvungu kwa uvungu ili chama chao kiweze kushinda.
Aliomba baraka, dua na maombi ya wazee na kusema kuwa anaamini wakimpa vitu hivyo atashinda katika uchaguzi mkuu ujao.
Huku akimtolea mfano hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema wakati baba huyo wa Taifa alipofika Dar es Salaam kuanzisha harakati za kupigania uhuru wa nchi, alishirikiana na wazee wa mkoa huo jambo ambalo lilimsaidia kupata nguvu ya kuwang’oa wakoloni.
“Ninatosha sana… ninatosha mbele, nyuma na ubavuni na naamini kwa dua na sala za wazee pamoja na umoja wetu, tutafanya kampeni nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, shuka kwa shuka, uvungu kwa uvungu na tunapata ushindi kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Magufuli.
HISTORIA YAKE
Akitoa historia yake jinsi alivyofika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza akitokea nyumbani kwao Chato, Dk. Magufuli alisema mwaka 1978 alipita wakati anakwenda kujiunga na Shule ya Sekondari Mkwawa iliyoko mkoani Iringa kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita.
“Mwaka 1985, nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa kipindi cha miaka mitatu, niliweza kushirikiana na wenzangu bila ya matatizo yoyote na sikuwahi kuulizwa kabila langu wala dini yangu.
“Mwaka 1990 hadi 1995, niliajiriwa mkoa huu, sijawahi kuulizwa wewe ni kabila gani, wala unatokea wapi, niliishi na wananchi wengine kama kawaida hadi sasa… ninawashukuru wananchi wa Dar es Salaam kwa sababu ndio nilioishi nao kipindi chote cha miaka 20 tangu niajiriwe,” alisema.
Naye mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wanawake nchini kusimama pamoja na kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi mwaka huu.
Alisema wanawake ndio mama wa familia, hivyo basi wanapaswa kuhamasishana na kuhakikisha Oktoba 25, mwaka huu wanajitokeza kwenye vituo vya kupigia kura ili waweze kukichagua chama hicho.
Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Shabani Matutu, Grace Shitundu na Jonas Mushi.