NA MWANDISHI WETU
ZIKIWA zimesalia siku chache kabla ya kuikabili Simba katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Klabu ya Mbabane Swallows ya Swaziland umefanya marekebisho katika benchi lao la ufundi na kumkabidhi Kinnar Phiri kuwa kocha mkuu wa timu yao.
Phiri ambaye ni raia wa Malawi, aliwahi kuinoa Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuamua kuachana nayo.
“Tumempa kazi ya muda mfupi Kinnah ili aongoze timu yetu katika michuano ya kimataifa kwasababu kocha wetu anatumikia adhabu,” alisema Meneja wa Mbabane Swallows, Sandile Zwane.
Alisema Thabo Vilakati anatumikia adhabu ya kusimamishwa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), baada ya kukutwa na hatia ya kumshambulia mwokota mipira wakati wa mchezo.
Mabadiliko hayo yamekuja siku chake ikiwa kikosi hicho kinajiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo itavaana na Simba Jumatano iyajo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Zwane alisema wanaamini Phiri atawasaidia kuwapa mbinu za kuikabili Simba, kwakuwa anaifahamu kwa undani timu hiyo baada ya kufundisha Ligi Kuu Tanzania Bara.