30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Suleiman Matola kipenzi Msimbazi aliyegeuka muasi

NA SOSTSHENES NYONI-DAR ES SALAAM

HAKUNA ubishi, Suleiman Matola ana heshima kubwa katika Klabu ya Simba yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam.

Heshima aliyonayo Matola Simba inatokana na jinsi alivyojitoa kwa moto kuitumikia klabu hiyo nyakati zake akiichezea, ambapo alipata kuwa kiungo hodari na kuisaidia kutwaa mataji.

Hili lilisababisha uongozi wa Simba kumpa heshima ya kuwa nahodha wa kikosi chao.

Ikumbukwe pia ubora wa Matola uliishawishi klabu ya Super Sport ya nchini Afrika Kusini kumsajili kutoka Simba.

Hata hivyo, Matola, ambaye baada ya kustaafu soka aliamua kugeukia ukocha na kuzifundisha klabu kadhaa, ikiwamo ya sasa ya Lipuli inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa ana sura nyingine tofauti na anapotazamwa na mashabiki na wapenzi wa klabu ya Simba.

Tangu alipokabidhiwa jukumu la kuinoa Lipuli msimu uliopita kutoka mikononi mwa raia wa Uganda, Richard Amatre, timu hiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwa Simba kuvuna pointi tatu.

Rekodi zinaonyesha Lipuli  tangu iliporejea Ligi Kuu msimu uliopita na kuwa chini ya Matola, haijawahi kupoteza mchezo dhidi ya Simba, mbali ya kumalizika kwa sare.

Hili ndio linalowafanya mashabiki na wapenzi wa Simba wasahau kwa muda mazuri yote aliyowahi kuyafanya Matoka akiwa mchezaji wa timu yao na kumtazama kama mwanajumuiya aliyewaasi.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo, Simba ilifunga bao la kuongoza kupitia kwa kiungo James Kotei, lakini beki Asante Kwasi aliizawazishia Lipuli kwa mkwaju wa mpira wa adhabu.

Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa mzunguko wa pili kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, matokeo yalikuwa  sare ya bao 1-1.

Lipuli ilitangulia kuandika bao kupitia kwa Adam Salamba, kabla ya Simba kusawazisha dakika za majeruhi kupitia kwa aliyekuwa mshambuliaji wao raia wa  Burundi, Laudit Mavugo.

Ni katika mchezo huo, kiwango cha juu cha Salamba kiliwavutia mabosi wa Simba ambao waliamua kumsajili katika kikosi chao anachokitumikia msimu huu wa Ligi Kuu.

Matola na Lipuli yake imeendelea kuonekana kuwa mlima mrefu kwa Simba hata msimu huu wa Ligi Kuu.

Hilo lilidhihirika katika mchezo wa kati ya timu hizo uliopigwa juzi Uwanja wa Taifa, ambako dakika 90 zilimalizika kwa suluhu.

Huo ulikuwa mwendeleo wa sare timu hizo zinapokutana katika michezo ya Ligi Kuu.

Hatujui nini kitatokea timu hizo      zitakapokutana katika mchezo wa mzunguko wa pili mkoani Iringa, ni suala la kusubiri na kuona.
Akizungumzia sare ya juzi dhidi ya Simba, Matola anakiri kwamba, wapinzani wao ni timu imara, hivyo alipaswa kuisoma kwa kina ili kuhakikisha hapotezi mchezo na kama akilazimika basi iwe sare.

“Simba wanatumia viungo wengi sana, kwa mantiki hiyo, ili uweze kuwamudu unatakiwa na wewe kujaza viungo wa kutosha katikati.

“Baada ya kuwasoma niliingia na plani hiyo na kweli ilitusaidia, unaweza kuona licha ya kwamba hatukupata ushindi, lakini tuliwamudu na kutengeneza nafasi za kutosha, ingawa hatukuzitumia,” alisema Matola na kuongeza:

“Njia pekee ya kuimudu Simba ni kujaza viungo wa kutosha,  kinyume na hapo utawapa nafasi ya kutawala mchezo na mwisho itakugharimu.”

Matokeo ya juzi kati ya timu hizo yaliifanya Simba ishindwe kumfikia na hata  kumporomosha mpinzani wake Yanga, ambayo Ijumaa iliyopita iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC na kukwea nafasi ya pili katika  msimamo wa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 29.

Simba baada ya sare ya Lipuli, imesalia nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 27, Azam ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 33.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles