23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Pemba wazira, Unguja wachechemea

mtanzaniadaily .inddELIAS MSUYA, PEMBA

HATUA ya kupiga kura kisiwani Pemba jana ilifanyika kwa utulivu huku kukiwa na idadi ndogo ya wapiga kura wakati kwa upande wa Unguja watu walijitokeza ingawa  kwa idadi ambayo si ya kuridhisha.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutangaza  kususia uchaguzi huo wa marudio.

Uchaguzi huo wa marudio ulifanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,   kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 akidai kuwa ulikiuka sheria na taratibu.

CUF kilipinga kufutwa kwa uchaguzi huo kikidai kuwa kilikuwa kimeshinda na kikatangaza kutoshiriki marudio yake.

Kisiwa cha Pemba chenye majimbo 18 ya Uchaguzi ni ngome ya CUF na katika uchaguzi huo kilishinda  majimbo yote kwa nafasi za Ubunge na Wawakilishi.

Kutokana na kujitoa kwa CUF katika uchaguzi wa marudio, jana vituo vingi vya kupiga kura vilivyofunguliwa tangu saa 1.00 asubuhi, vilikuwa na watu wachache na ilipofika saa 5.00   vingi vilikuwa wazi huku baadhi ya wasimamizi wakijilaza kwenye madawati na meza.

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa wasimamizi katika kituo cha Wawi ‘A’, Ismail Issa, alisema kujitoa kwa CUF kumesababisha wananchi wengi wasipige kura.

“Watu ni wachache sana ikilinganishwa na uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 ambako kulikuwa na misururu ya watu wengi hadi saa 10.00 alasiri. Leo hadi saa 3.00 hii hakuna watu,” alisema Issa.

Alisema kituo hicho chenye wapiga kura 1400 kilitarajia kupata asilimia 20 ya wapiga kura.

Akizungumzia hali hiyo, Mgombea urais wa Chama cha ADC, Hamad Rashid, alisema kisiwa hicho ni ngome ya CUF ingawa akisema kujitoa kwao hakutaathiri utendaji wa Serikali.

“Hii ni ngome ya CUF, kisiwa hiki kina majimbo 18 na yote waliyachukua, lazima tukubali hilo, ndiyo maana waliojitokeza leo ni wachache. Lakini hakuna athari yoyote ya kujitoa kwao.

“Mwaka 2003 tulipiga kura ya maruhani, walioshinda walipata mamia ya kura na walioshindwa wakiwa na maelfu, lakini Serikali iliendelea,” alisema Rashid.

Rashid alisema ameamua kushiriki uchaguzi huo kwa kuwa ni haki yake na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi na wasiotaka wasiwabugudhi wengine.

“Tunataka kupata Serikali, tunataka kuingia kwenye maendeleo. Tatizo letu kubwa ni ajira kwa vijana wanaokaa vijiweni.

“Ndiyo maana namuunga mkono Rais John Magufuli kwa kauli yake ya Hapa Kazi tu na sisi ADC tunasema Hapa ni Wajibu Tu,” alisema Hamad,

Hamad Rashid,  anatajwa kuwa huenda ndiye akawa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mgombea urais huyo wa ADC,  alisema kwamba hakuna chama kidogo kwenye siasa na lolote linaweza kutokea.

“Hakuna chama kidogo. Mwaka 1963 kulikuwa na vyama vya ASP na ZNP vilivyopata viti 10 kila kimoja huku chama cha ZPPP kikipata viti vitatu.

“ ZPPP kiliungana na ZNP na kiongozi wake ndiye akawa Waziri Mkuu. Kwa hiyo mambo hubadilika, unaweza kusikia Hamad akawa Rais,” alisema.

Ingawa alikiri kuwapo   matatizo katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), aliendelea kutetea chama chake kushiriki uchaguzi huo akisema ndiyo njia bora ya kurekebisha kasoro.

“Hivi ukiumwa na mkono ndiyo uukate?  Hapana utautibu. Mbona hao wanaoikosoa ZEC hawatoki? Ni wanachama wa CUF lakini hawatoki. Huwezi kuirekebisha ZEC bila kuwa na Baraza la Wawakilishi,” alisema.

Mbali na Hamad Rashid, mgombea urais mwingine aliyefika kupiga kura kwenye kituo hicho alikuwa Mwenyekiti wa AFP, Said Soud Said aliyejipa matumaini ya kushinda.

“Nashukuru tumepiga kura na Mungu ameleta manyunyu, hii ni ishara ya neema. Hata siku ya kiama kutakuwa na manyunyu. Watu wamepiga kura na watapata kiongozi mpya ambaye ni mimi.

“Kujitoa kwa CUF hakutaathiri chochote kwa sababu hata mwaka 2003 walipiga kura za maruhani lakini Serikali ikaendelea tu,” alisema Said.

Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Zanzibar, Mohamed Aboud, aliyekuwa akizunguka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, alikiri kuwapo   idadi ndogo ya wapiga kura lakini akasema wanatarajia kupata angalau asilimia 40.

‘Nawashukuru wananchi kwa kujitokeza kupiga kura, natoa wito waendelee kupiga kura. Ni kweli kuna uchache wa watu, lakini hauleti mshtuko kwa sababu kila upande una wanachama wake.

“Hapa Pemba kuna wanachama wengi wa CUF na kule Unguja kuna wanachama wengi wa CCM. Tunatarajia kupata angalau asilimia 40 ya wapiga kura,” alisema Waziri Aboud.

Katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, hali ya usalama ilikuwa shwari   huku idadi ya watu waliojitokeza ikiwa ndogo zaidi.

Wasimamizi wapiga usingizi

Baadhi ya wasimamizi katika kituo cha Shule za Kizimbani na Kunjwi walionekana kulala kwenye meza kwa kukosa wapiga kura huku polisi wakijipumzisha kwenye viti.

Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Khalid Rashid,    alisema hali ya usalama imeimarishwa na wapiga kura wamejitokeza.

“Hali ya usalama iko shwari   na vijana tuliowatarajia wamekuja kupiga kura. Hata hivyo, ikilinganishwa na uchaguzi wa Oktoba 25, waliopiga kura sasa siyo wengi,” aliema Rashid.

Katika vituo mbalimbali, CCM iliweka mawakala watatu wanaowakilisha Rais, Mbunge na Diwani, huku vyama vingine vya ADC na Tadea vikiwa na wakala mmoja mmoja.

Usalama

Hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa katika maeneo mengi huku magari yaliyosheheni polisi na magari ya Jeshi la Wananchi  wa Tanzania (JWTZ) yakiranda mitaani.

Vilevile,  mitaa mingi haikuwa na watu na maduka na hoteli nyingi zilikuwa  zimefungwa.

Mwisho

 

 

Vyombo vya ulinzi waranda Unguja

NA SARAH MOSSI, ZANZIBAR

VYOMBO vya usalama vilidhibiti hali ya usalama huku idadi ndogo ya wapiga kura wakijitokeza jana katika uchaguzi wa marudio mjini Unguja.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi na ilipofika  saa 1.00  watu walianza kupiga kura ingawa hakukuwa na misururu ya watu kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25, mwaka jana

 

Idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura  iliendelea kupungua hasa   mchana na baadaye  alionekana mtu mmoja mmoja  akijitokeza kwenye vituo.

Baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi kwenye vituo mbalimbali walionekana wakali   na hata walipoulizwa baadhi ya maswali walijibu kwa mkato wakisema wao siyo wasemaji wa tume.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Salum Kassim Ali, alipoulizwa jana kuhusu kuonekana idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo, alikataa kukiri  na kumtaka mwandishi kufanya utafiti juu ya hilo.

“Kuwaona watu katika maeneo ya kupiga kura siyo wote wapiga kura na si lazima wote wapige kura, hebu fanya utafiti kwanza,” alisema Ali.

Idadi ya wapiga kura wote Zanzibar ilikisiwa ni watu 5,583.

Viongozi warusha vijembe

Mapema saa 1.00 asubuhi, Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, akiwa ameongozana na mkewe, Mwanamwema Shein, walipiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Bungi, Kituo cha Kibele.

Dk. Shein pia aliongozana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), January Makamba.

Akijibu maswali ya wanahabari baada ya kumaliza   kupiga kura, Dk. Shein, alisema amefurahishwa na idadi ya watu waliojitokeza  na kusisitiza anaamini uchaguzi umekwenda vizuri.

Alipoulizwa anajisikiaje iwapo atashinda kwenye uchaguzi huo uliosusiwa na  wenzao wa Chama Cha Wananchi (CUF), Dk. Shein alijibu hilo kwake halioni kama ni tatizo kwa sababu  waliingia wenyewe na wamejitoa wenyewe.

“Mradi wananchi wamejitokeza kupiga kura wao kususia haitushughulishi, waliingia wenyewe na wamejitoa wenyewe,” alisema Dk. Shein.

Balozi Seif

Naye Makamu wa Pili wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Taifa (SUK), Balozi Seif Ali Iddi, alifika katika kituo cha kupiga kura cha Shule ya Msingi Kitope  saa 2:22 asubuhi akiwa ameongozana na mkewe, Asha Iddi.

Akizungumza na waandishi   baada ya kumaliza kupiga kura, Balozi Seif alisema amefurahi kuona nchi iko shwari na watu wamejitokeza   kupiga kura.

“Hii ni salamu zao kwamba nchi iko shwari na hili limenifurahisha  kwa sababu  watu wamejitokeza kupiga kura kama mnavyowaona,” alisema.

Samia apiga kura

Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alifika katika kituo cha kupiga kura  katika Shule ya Msingi Kiembe Samaki  4:05 asubuhi.

Baada ya kumaliza kupiga kura, aliwaambia waandishi wa habari  kwamba amefurahishwa  kuona idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza hususan kinamama, lakini pia alifurahishwa na hali ya utulivu aliyoiona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles