MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Brazil na klabu ya Sport Club Corinthians Paulista, Alexandre Pato, amefurahia kumalizana na Chelsea kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo kwa mkopo.
Mchezaji huyo atakuwa wa kwanza kusajiliwa na klabu hiyo chini ya kocha wao, Guus Hiddink, katika kipindi hiki cha usajili wa Januari na tayari amewasili jijini London kwa ajili ya vipimo ili waweze kumalizana na nyota huyo mwenye umri wa miaka 26.
“Nina furaha kubwa kuwa mchezaji wa Chelsea, hii ni klabu ambayo nilikuwa na ndoto nayo, hapa naweza kusema kuwa ni sawa na nyumbani kwangu. Nawashukuru mashabiki wa Chelsea na wale wote wanaoniunga mkono popote niendapo.
“Nimepata ujumbe mbalimbali kutoka kwa marafiki zangu kwenye mtandao wa Instagram, Twitter na Facebook ambazo zinanipa faraja kubwa katika maisha yangu ya soka.
“Lengo langu kubwa ni kucheza soka, sijui niseme nini kwa kuwa nina furaha kubwa, najua kwamba ninazidi kujiongezea idadi kubwa ya mashabiki, hasa katika klabu hii ya Chelsea ambayo nilikuwa ninaitamani katika maisha yangu ya soka,” alisema Pato.
Nyota huyo aliwahi kukipiga katika klabu ya AC Milan kwa miaka mitano kati ya 2007 hadi 2012, kabla ya kurudi nchini Brazil katika klabu hiyo ya Corinthians mwaka 2013.