HERIETH FAUSTINE NA ESTHER MNYIKA
WASANII wa ndani na nje ya nchi wanatarajia kutumbuiza katika tamasha la Karibu Music Festival 2015 huku mgeni mwalikwa akiwa ni mwanamuziki kutoka Congo, Papa Wemba.
Wasanii wengine wanaotarajiwa kutumbuiza katika tamasha hilo ni Jhikolaman, Isha Mashauzi, Damian Soul, Juma Nature, Barnaba, Shilole, mshindi wa pili wa BSS, Nassib Fonabo na bendi yake ya Spirit na wengine wengi.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 6 hadi 8 katika viwanja vya Mwanakalenge, Bagamoyo mkoani Pwani likiwa na lengo la kukuza muziki wenye asili ya Afrika.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya watayarishaji wa muziki ya Legendary kwa kushirikiana na kampuni ya kinywaji cha Jebel Coconut.
Mratibu wa tamasha hilo, Ernest Biseko, alisema wameandaa tamasha hilo kwa lengo la kuonyesha utamaduni za Kiafrika kwa dunia nzima kupitia jukwaa la muziki kwa kuwa litakutanisha wanamuziki kutoka mataifa mbalimbali.
“Tamasha hili litakuwa la pili kufanyika na litakuwa sehemu ya kukutanisha wadau wote wa muziki kutoka dunia nzima ili kubadilishana uzoefu wa kikazi na kufungua milango kwa wasanii ili watengeneze mtandao wa soko la kimataifa,” alisema Biseko.
Tamasha hilo linadhaminiwa na Swiss Embassy, Precion Air, Coca Cola, Mwananchi Communication, Kaya fm, Magic fm, Focus Outdoor, Jovago, Kaymu na Time tickets.