24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Papa Wema afarii akifanya anachokipenda

papa wembaNA NOAH YONGOLO

HAKIKA ni habari ya kushtua sana na kuhuzunisha barani Afrika na dunia nzima kwa kifo cha ghafla cha mwanamuziki maarufu, Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba maarufu kwa jina la Papa Wemba au Le Grand Muzee.

Amefariki juzi akiwa kazini kwenye jukwaa wakati akifanya onyesho katika tamasha la muziki liitwalo Femua jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

Tukio hili lilitokea wakati wanamuziki wake wakiendelea kutumbuiza kabla ya mmoja wao kumwona akidondoka na kisha kusaidiana na wenzake kujaribu kumwokoa akiwa anatetemeka na hatimaye kupoteza fahamu.

Msemaji wa nguli huyo aliyefahamika kwa jina la Henry Christmas Mbuta Vokia, alisema marehemu Papa Wemba alikuwa amepanda jukwaani muda mfupi na kutumbuiza wimbo mmoja huku mashabiki wake wakimtaka arudie wimbo huo na alifanya hivyo.

Baada ya kuanza kuupiga tena wimbo huo na kuongeza wimbo wa tatu hatimaye alianguka chini na kupoteza fahamu.

Juhudi kubwa zilifanyika na watu wa huduma ya kwanza kwa ajili ya kutaka kuokoa maisha ya msanii huyo kwa kumpeleka hospitali lakini hazikuzaa matunda.

Baada ya kumfikisha hospitalini nusu saa baadaye alifariki dunia. Historia ya marehemu Papa Wemba ni ndefu sana na ilianza miaka ya 66 iliyopita pale alipozaliwa mjini Lubefu, Mkoa wa Kasai Oriental mwaka 1949.

Baada ya baba yake kufariki mwaka 1966 alianza rasmi kazi ya muziki kwa kujiunga na kwaya ya kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Kinshasa.

Mwaka 1969, akiwa na vijana wenzake; Pepe Felix Manuaku, Nyoka Longo Jossart, Evoloko, Mavuela Simon, walianzisha bendi ya Zaiko Langalanga, utunzi wake wa kwanza ni wimbo Madrigal, ukifuatiwa na tungo nyingine kama Mete ya Virite, Chouchouna, Amazone na nyingine nyingi.

Alipitia katika bendi nyingi zikiwemo Isifi Lokole, Yoka Lokole, Afrisa International ambapo walitoa vibao vikali vilivyopendwa kama Matembele bangi na Maloba Bakoko.

Mwaka 1977, aliunda bendi yake mwenyewe ya Viva la Musica ambayo mpaka mauti yanamfika alikuwa akiendelea kuiongoza. Miaka miwili ya mwanzo katika bendi hiyo walitoa nyimbo nyingi zilizotamba kama vile Superieure, Ebale Mbonge, Mabele mokonzi, Bakulaka, Ekoti ya nzube, ambazo alishirikiana na wanamuziki; Kisangani Esperant, Pepe Bipoli, Jadot Le Comodgien, Petit Aziza, Kester Emeneya, Rigo Star, Bongo Wende, Syriana, Pinos na Albert William Longomba (Awilo).

Katika uhai wake, Wemba alianzisha kijiji chake kilichokuwa na masharti na kanuni zake ndani ya uwanja wao wa familia jijini Kinshasa alichokiita Molokai Village yeye akiwa kiongozi wake.

Mwanzoni mwa miaka ya 80 alitokea kuwa maarufu sana nchini mwake na kupendwa na vijana, wakimwita Sape (kiongozi mkuu wa vijana watanashati), aliendelea kutoa vibao motomoto kama Signorina, Analengo, Mea Culpa, Melina La Parisienne, Santa, Matebu na nyingine nyingi.

Mwaka 80 mwishoni, alihamia nchini Ufaransa na kufanikiwa kutoa albamu kama Mfono Yami, Le Voyageur, Foridoles na Malimba.

Wemba alishirikiana na wanamuziki mbalimbali ulimwenguni kama vile marehemu Tabule Ley, Martin Meissonier, Peter Gabriel, Manu Dibango, Ray Lema, Koffi Olomide, Yousou Ndour, Pepe Kalle, Alpha Blond, Aretha Franklin, Salif Keita na wengine wengi.

Zaidi ya miaka 40 katika kazi za muziki, ameweza kumiliki bendi nne hadi umauti unamkuta zikiwemo, Viva la musica, Viva la musica Cour Des Grands, Nouvelle Ecriture na Viva Tendances.

Katika uhai wake alifanikiwa kupata tuzo nyingi pamoja na iliyomletea heshima kubwa mara baada ya kuachia albamu yake ya Emotion mwaka 1995, tuzo hiyo ilijulikana kwa jina la Disc D’Or iliyotolewa nchini Marekani.

Mbali na muziki, Wemba aliwahi kucheza filamu mbalimbali kama vile La Vie est Belle, Combat De Fauvest na Kinshasa Kids.

Juni 2003, alihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja na miezi mitatu na mahakama ya nchini Ubelgiji kwa tuhuma za kuwaingiza raia wa Zaire sasa DRC) barani Ulaya kinyume cha sheria, hata hivyo mahakama hiyo ilimtaka alipe faini ya Euro 22,000.

Lakini mdhamini wake alitoa Euro 30,000 ili aweze kutumikia kifungo cha miezi michache ambapo alikaa miezi mitatu jela.

Alipotoka jela alitunga wimbo Numero D’ Ecrou, ambao ulikuwa unasimulia kwamba alikutana na Mungu gerezani.

Hakika Wemba ameacha pengo kubwa katika muziki wa Congo kwani wamepoteza mwalimu, mwanamitindo na mtunzi mahiri kati ya waliowahi kutokea.

Dunia itamkumbuka mwanamuziki huyo kutokana na kile alichokifanya katika maisha yake ya muziki. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles