30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

PAPA FRANCIS: MATESO YA WAROHINGYA YALINILIZA

VATICAN CITY, VATICAN


PAPA Francis alifichua kuwa alilia baada ya kusikia masaibu ya wakimbizi wa jamii ya Rohingya nchini Bangladesh.

Akizungumza na wanahabari wakati akirudi mjini Roma juzi, Papa Francis pia aliongeza kuwa mkutano wake na jamii hiyo ulikuwa moja ya masharti ya ziara yake nchini Myanmar na Bangladesh na kwamba wakimbizi hao pia walilia.

Mkutano wake na Warohingya ulikuwa ishara muhimu ya kuonyesha kuunga mkono jamii hiyo ya Waislamu walio wachache wanaotoroka ghasia Myanmar.

“Nilijua nilikuwa nikienda kukutana na Warohingya, lakini sikujua ningekutana nao wapi na vipi, kwangu kuonana nao ilikuwa moja ya masharti ya ziara yangu,” alisema.

Papa huyo mwenye uwazi katika mambo yake, alikuwa na wakati mgumu kudumisha itikadi za kidiplomasia kwenye ziara yake ya siku nne nchini Myanmar.

Katika ziara hiyo ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Kanisa la Katoliki duniani katika nchi hiyo, alijikaza kutowataja moja kwa moja Warohingya hadharani badala yake akiwaomba viongozi wa Buddha kukomesha ubaguzi na chuki.

Akiwa Bangladesh, alishughulikia suala hilo waziwazi, na kukutana na kundi la wakimbizi wa Rohingya kutoka kambi zilizo kusini mwa nchi hiyo mjini Dhaka.

Akiwa Myanmar, Papa Francis alikuwa ametahadharishwa na Askofu Mkuu wa Yangon kutolitaja jina hilo nchini humo ili kuzuia taharuki na kuhatarisha maisha ya Wakristo.

Ni kwa vile jina hilo halitajwi katika nchi hiyo ya Wabuddha wengi, kwa sababu hawaitambui Rohingya kama jamii wakisema ilitoka Bangladesh.

“Kama ningetumia neno hilo kwenye hotuba yangu rasmi, ningekuwa nimefunga mlango wa majadiliano. Walikuwa wakielewa mawazo yangu. Kilicho muhimu kwangu ni kwamba ujumbe uliwafikia.

“Kuhusu Bangladesh, yale ambayo wamewafanyia wakimbizi hawa ni makubwa, na mfano wa kuigwa.

“Nililia, nilifanya hivyo kwa njia ambayo nisingeonekana… Walilia pia, nilijiambia, siwezi kuondoka bila kuwaambia neno lolote,” alisema.

Papa Francis aliwaambia Warohingya: “Katika jina la wote waliowatesa na waliowajeruhi, ninawaomba msamaha wenu.”

Wakimbizi zaidi ya 620,000 wa Rohingya wamekimbilia Bangladesh wakitoroka msako wa wanajeshi nchini Myanmar.

Wamesimulia mateso, ubakaji, mauaji na vijiji vyao kuchomwa moto na wanajeshi na wanamgambo wa Kibuddha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles