VATICAN CITY,Vatican
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Buniani, Papa Francis, amesema mapenzi ya jinsia moja kwa makasisi ni tatizo kubwa na ambalo linampa hofu.
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo katika mahojiano na mmisionari kutoka Hispania kuhusu wito wa dini ambayo ni sehemu ya kitabu kinachoandikwa na mmisionari huyo.
Katika mahojiano hayo, Papa Fransis alisema uhusiano wa jinsia moja ni jambo lisilofaa na ametaka makasisi kutii viapo vyao vya utawa.
Gazeti la Corriere della Sera la Italia limechapisha sehemu ya mahojiano hayo katika mtandao wake juzi na katika moja ya sehemu hiyo, Papa Francis alisema Kanisa Katoliki linapaswa kuwa imara wakati wa kuchagua watu watakaokua makasisi.
“Hili suala la uhusiano ya mapenzi ya jinsia moja ni kubwa sana,” alisema Papa Fransis na kusisitiza kuwa wote wanaohusika na mafunzo kwa makasisi wahakikishe wanafunzi wao wamekomaa kama binadamu na kwa hisia kabla ya kuwapatia Sakramenti ya Upadrisho.
“Kwa sababu hiyo, Kanisa linawataka watu wenye tabia hizo za mapenzi ya jinsia moja wasikubaliwe katika maisha ya ukasisi,”alisema kiongozi huyo.
Alisema agizo hilo pia linawahusu wanawake ambao wanataka kuwa watawa wa kanisa hilo.
“Katika jamii zetu, sasa inaonekana suala hili la mapenzi ya jinsia moja limekuwa fasheni. Mawazo kama hayo sasa yanaanza kupata ushawishi ndani ya kanisa,” alisema Papa na kuongeza kuwa suala hilo katu halina nafasi katika maisha ya watawa wake.
Mwaka 2013, Papa alisisitiza juu ya msimamo wa kanisa hilo kuwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni dhambi.
Kuhusu uhusiano binafsi wa Mungu na mtu mwenye kujihusisha na vitendo hivyo alijibu; “Kama mtu ni shoga na anataka ukaribu na Mungu na ana nia njema, mimi ni nani wa kuhukumu?”
“Nguvu ya Utumishi”, ni kitabu kilichotungwa na Padre Fernando Prado baada ya mahojiano ya saa nne na Papa kuhusu changamoto za kuwa kasisi na kinatarajiwa kuchapishwa wiki hii.