NA VERONICA ROMWALD
– DAR ES SALAAM
PACHA wa kike waliozaliwa Julai 21, mwaka huu huko mkoani Morogoro wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo, watatenganishwa.
Watoto hao hivi sasa wapo chini ya uangalizi maalumu wa jopo la madaktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako walifikishwa tangu Julai 24, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo kuhusu maendeleo ya hali zao, daktari bingwa wa upasuaji wa watoto wa MNH, Zaituni Bukhari, alisema watoto hao wana afya nzuri.
“Inawezekana kuwafanyia upasuaji wa kuwatenganisha, vipimo vya awali tulivyofanya vimeonyesha kila mmoja ana mfumo wake wa damu na vile viungo muhimu, kwa mfano moyo, figo, ini na utumbo kila mmoja ana kiungo chake.
“Hata hivyo, katika ini na moyo vipimo vimeonyesha kuna vitu wanashirikiana, kwa mfano kwenye moyo imeonekana wanashirikiana baadhi ya chemba,” alisema.
Dk. Bukhari alisema Muhimbili wanao uwezo wa kuwafanyia upasuaji watoto hao ingawa kulingana na uzoefu na utaalamu zaidi, nchi zenye uwezo wa kuwafanyia kwa uwezo wa hali ya juu ni India na Saudi Arabia.
“Wanaweza kutenganishwa na wanakuwa salama kabisa, lakini upasuaji huo haiwezekani kufanyika wakiwa chini ya umri wa miezi sita kwa sababu chini ya hapo miili yao inakuwa bado haijaweza kuhimili zile dawa za usingizi na upasuaji wenyewe ambao huchukua hadi saa 20 kumalizika,” alisema.
Dk. Bukhari alisema upasuaji huo huusisha jopo la madaktari wasiopungua 10, wakiwamo madaktari bingwa wa watoto, madaktari bingwa wa vifua, moyo, ini, usingizi, upandikizaji ngozi na wengine.
“Kwa mujibu wa ripoti ya awali ya daktari ambako mama alijifungua, inaonyesha walizaliwa na kilo 4.270, walikuwa na maambukizi kidogo kwenye kitovu, mmoja alikuwa anapumua kwa shida kidogo na mmoja alikuwa amevunjika katika sehemu ya mfupa wa paja,” alisema.
Daktari huyo alisema ingawa kitaalamu haijajulikana nini hasa husababisha watoto kuzaliwa wakiwa wameungana, hata hivyo alisema vipo baadhi ya vitu ambavyo huchochea hali hiyo.
“Mama akizaa watoto wengi, akikosa madini ya calcium, chuma na virutubisho vingine ambavyo hupatikana kwenye aina fulani ya vyakula, madini ya folic acid, uzazi wa pacha huweza kuchangia mama kupata mtoto wa aina hii,” alisema.
Alishauri wanawake kuhudhuria kliniki mara tu wanapojihisi kuwa ni wajawazito kwani huko watafanyiwa uchunguzi na kuna ushauri muhimu ambao hutolewa.
Mama wa pacha hao, Rebeka Muya, alisema amepokea kwa furaha taarifa hiyo ya madaktari kuwapo uwezekano wa watoto wake kutenganishwa.
“Ni ujauzito wangu wa tisa, tayari nina watoto wanane, hivyo sasa nina watoto wa kiume wanane na wa kike wawili, nashukuru Mungu familia yangu bado ipo pamoja na mimi na inanijali,” alisema mama huyo.