26.9 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

PAC yaamuru vigogo Bandari wakatwe mishahara

Pg 3 jan 16Fredy Azzah
WATUMISHI wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wamebainika kujilipa mamilioni ya posho kwa ajili ya safari kwa takribani miaka mitatu, bila kibali cha Msajili wa Hazina kama taratibu zinavyotaka.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeagiza menejimenti ya TPA kuwakata mishahara wafanyakazi wote ambao kwa nyakati tofauti wamelipwa fedha hizo.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema kwa safari za ndani ya nchi, TPA imekuwa ikilipa watumishi wake posho ya Sh 500,000 kwa siku kwa watumishi wa ngazi za juu, huku wale wa chini wakilipwa Sh 125,000 kwa siku.
Alisema viwango vya awali vya posho kwa watumishi hao, ilikuwa ni Sh 270,000 kwa siku kwa watumishi wa ngazi za juu na wale wa chini walikuwa wakilipwa Sh 95,000.
Alisema kwa safari za nje, watumishi hao wanalipwa Dola za Marekani 800 kwa siku, huku kiwango cha zamani kikiwa dola 600.
“Kibali cha Msajili wa Hazina kimetoka Januari2, mwaka huu, nyie kwa muda mrefu mmekuwa mkilipana fedha ambazo hazijaidhinishwa na TR, (Msajili wa Hazina), kamati inawaagiza, watumishi wote waliolipwa viwango vipya kabla ya kibali cha hazina wakatwe mishahara yao na fedha za umma zirudi” alisema Zitto.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema kiasi hicho kimekuwa kikilipwa kwa watumishi hao tangu mwaka 2011.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Madeni Kipande aliiambia kamati hiyo kuwa baadhi ya watumishi waliolipwa fedha hizo, wamefariki dunia na wengine wamestaafu.
Kutokana na kauli hiyo, Zitto alisema. “Sisi tumetoa agizo tunachotaka ni utekelezaji, ambao wamekufa ama kustaafu mtaleta ripoti na ambao wapo ikiwa ni hata nyie hapo kwa sababu mmesafiri kwa fedha hizi tunataka mkatwe mishahara yenu.
“Wale wote waliosafiri kwa kutumia fedha hizo kabla ya Januari 2 kibali kilipotoka wakatwe mishahara,” alisema Zitto.
Mara ya mwisho PAC kukutana na TPA, ilimwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Joseph Msambichaka kutoa maelezo ya matumizi ya Sh bilioni 20 zilizotumika katika mkutano wa wafanyakazi, matangazo na safari za ndani na nje za vigogo.
Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema alipopata ripoti ya TPA na kupitia kwa haraka haraka, alibaini uwepo wa matumizi mabaya ya fedha za walipakodi baada ya kubaini mamlaka hiyo ilitumia Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya mkutano wa siku moja kwa wafanyakazi wake.

Alisema fedha nyingine zilizotumika kwa matumizi mabaya ni Sh bilioni 6.4, zilizotumika kwa ajili ya matangazo na Sh bilioni 10 kwa ajili ya safari za nje na ndani kwa ajili ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Katika kikao cha jana, PAC ilikuwa ikipitia taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu matumizi ya Sh bilioni 9.6 zilizotumika kwa ajili ya vikao vya baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo, matumizi ya Sh bilioni 6.4 zilizotumiwa katika matangazo kwa vyombo vya habari.
Suala jingine, lilikuwa ni Sh bilioni 10 zilizotumika kwa ajili ya safari za ndani na nje ya nchi.
Hoja hizo zilibainika katika hesabu za TPA za mwaka 2011/12. Baada ya wajumbe wa PAC kuchambua hesabu hizo, walibaini baadhi ya maeneo mamlaka hiyo imekosa nyaraka za kuthibitisha matumizi ya fedha walizotumia.
Kutokana na hali hiyo, Mhandisi Kipande alisema wamekuwa wakipata shida kupata nyaraka hizo, lakini kila wanapowabana watumishi wao, wanapata baadhi ya nyaraka.

Kauli hiyo ilifanya Filikunjombe kuhoji kwa nini nyaraka hizo zipatikane baada ya watumishi kubanwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles