26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

OZIL, SANCHEZ WANAVYOMWENDESHA WENGER KAMA GARI BOVU   

NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


mesut-ozil-na-alexis-sanchezKOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, kichwa kinamuuma kila anapofikiria jinsi wachezaji wake nyota wawili, Mesut Ozil na Alexis Sanchez, wanavyomwendesha mbio kama gari bovu.

Kutokana na hilo, Arsenal itaingia gharama zaidi ya pauni milioni 36, baada ya kushindwa kumalizana mapema na nyota hao, kwa kuwapa mkataba mpya katika usajili wa majira ya joto.

Inadaiwa mastaa hao kila mmoja anataka kulipwa mshahara wa pauni 290,000 kwa wiki, ili kuweza kuendelea kubaki uwanjani Emirates.

Nyota hao  wawili tayari wameiweka klabu hiyo katika wakati mgumu, kwani wanahitaji dau nono ambalo si rahisi kupewa na klabu hiyo.

Wenger amekiri kuwa klabu inapata wakati mgumu kufikia makubaliano kati ya Ozil na Sanchez kuongeza mkataba wao kwa sasa.

Mazungumzo baina ya Gunners na wachezaji hao nyota ambao watakuwa wamemaliza mkataba wao ifikapo mwisho wa msimu ujao, yamesemekana kugonga mwamba wiki iliyopita.

Wenger hivi karibuni alidai kuwa anahitaji kiasi cha fedha cha kutosha kukidhi madai ya mshahara wa wawili hao, lakini kutokana na klabu nyingine kutaka huduma za wachezaji hao, Mfaransa huyo hana uhakika kama watakubali kusaini mkataba mpya.

“Daima ni vigumu, kilichobadilika ni namba, lakini ni vigumu mara zote kubakisha wachezaji bora kwa sababu wanatakiwa na klabu nyingine.

“Wachezaji wanataka dau nono kwa sababu wana muda wa miaka 10 tu kucheza soka katika kiwango cha juu.”

Ozil ndiye mchezaji anayelipwa vizuri zaidi Arsenal, akipokea mshahara wa pauni 140,000 kila wiki, wakati Sanchez akichukua pauni 130,000 kwa wiki.

Hata hivyo, Wenger anasema Arsenal haitawauza wachezaji hao,  hata kama hawatasaini mikataba mipya.

Wawili hao msimu huu wameifungia Arsenal jumla ya mabao 21, hata hivyo Wenger amesema: “Hata iweje watabaki kwa miezi 18 iliyobaki na labda zaidi ya hapo.”

Aliongeza: “Wachezaji hawa watabaki si chini ya miezi 18, mazungumzo yanaendelea, lakini siwezi kuweka wazi.”

Ingawa Wenger ana matumaini ya kubakia kwa Ozil na Sanchez, lakini ameshindwa kuwapa uhakika wowote mashabiki wa Arsenal.

Alipohojiwa kama anawapa uhakika mashabiki kuhusu kubakia kwa wawili hao, Wenger alijibu: “Hapana wana miezi 18 ya mikataba yao na wataendelea kucheza wakiwa hapa, baada ya hapo itabidi mikataba iongezwe, lakini siwezi kuzungumzia suala hilo katika kila mahojiano na wanahabari. Ni kawaida mkiongeza mkataba kuna majadiliano.”

Hivi sasa Sanchez anahusishwa kuhamia huko Mashariki ya mbali, hasa China ambako imeripotiwa amepewa ofa ya kulipwa pauni 400,000 kwa wiki.

Wenger amepasua: “Naamini hilo, lakini kwanini uende China wakati leo unacheza England?” alihoji Wenger.

Wawili hao inasemekana wanadai mshahara mpya ambao unakadiriwa kuwa sawa na ule wa Pogba wa pauni 290,000 kwa wiki.

Lakini Arsenal haipo tayari kukidhi mahitaji yao hayo, badala yake wanaandaa kiasi kinachokadiriwa kufikia pauni 200,000 kwa wiki, ambacho kitazidi mshahara wa sasa wa Arsene Wenger unaoripotiwa kuwa pauni 160,000.

Sababu mbili zinazoumiza kichwa cha Wenger kwa wachezaji hao ni muda uliobaki kwenye mikataba yao kuelekea mwaka mmoja na kuzua hofu ya kuondoka bure.

Nyingine ni mfumuko wa bei katika mishahara ya Ligi Kuu England, kutokana na dili jipya la matangazo ya runinga mpango ambao umeleta athari mwanzoni mwa msimu.

Mbali na mastaa hao, Santi Cazorla pia mkataba wake unakaribia kumalizika ambapo unatarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu, bodi ya Arsenal imejaribu kufanya mazungumzo mara kadhaa, lakini imekuwa ikirudishwa nyuma katika mazungumzo hayo na Ozil na Sanchez.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles