LONDON, ENGLAND
KIUNGO wa vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool, Alex Oxlade-Chamberlain, atarejea uwanjani kuungana na wenzake Februari mwakani baada ya kupona kifundo cha mguu.
Kiungo huyo aliumia kifundo cha mguu Aprili mwaka huu akiwa katika mchezo wa nusu fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Roma.
“Ni taarifa nzuri kwetu, ameanza kwenda kutazama baadhi ya michezo na anaonekana kuwa imara, tunatakiwa kusubiri,” alisema Jurgen Klopp.
“Hakuna presha Februari au Machi si mbali tusubiri kurejea uwanjani,” alisema.
Oxlade-Chamberlain anatakiwa kufanyiwa upasuaji baada ya kuvaana na beki wa Roma, Aleksandar Kolarov, ambao Liverpool ilishinda mabao 5-2 katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa uliochezwa England.
Nyota huyo wa timu ya taifa ya England alianza kukosekana uwanjani tangu michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Juni mwaka huu nchini Urusi.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Arsenal, aliposti katika ukurasa wake wa Instagramu: “Hisia zinazomtokea mtu akiwa njiani kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka nane.”