26.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Yanga yawapa mashabiki wao zawadi ya Mwaka mpya

MWANDISHI WETU-MBEYA

MSHAMBULIAJI Heritier Makambo, ameendelea kuwasha moto baada ya jana kufunga mabao mawili wakati timu yake ya Yanga ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 50 na kuendelea kujikita katika uongozi wa ligi hiyo, baada ya kushuka dimbani mara 18, ikishinda michezo 16 na kutoka sare mbili.

Makambo alifunga mabao yake hayo dakika ya 16 na 41, huku bao pekee la Mbeya City lilipachikwa na Idd Seleman ‘Ronaldo’, dakika ya 39.

Makambo alifunga bao la kwanza kwa kuusindikiza mpira wavuni kwa kifua baada ya kuunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Ibrahim Ajib. Faulo hiyo ilitokana na mmoja wa wachezaji wa Mbeya City kumfanyia madhambi beki wa Yanga, Gadiel Michael.

Mshambuliaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alifunga bao la pili kwa kichwa baada ya kuunganisha pasi ndefu ya Paul Godifrey, hivyo kufikisha mabao 11 msimu huu.

 Seleman aliisawazishia Mbeya kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Erick Kyaruzi.

Mwamuzi wa mchezo huo, Martin Saanya, aliwalima kadi za njano Haruna Moshi ‘Boban’, Makambo, Kelvin Yondan na Ramadhan Kabwili wa Yanga kutokana na kuonyesha mchezo usiofaa, wakati kwa upande wa Mbeya City, Mohamed Kapeta, alilimwa kadi ya njano.

Mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo kila upande ulionekana ukiwa na uchu wa kutaka kuandika bao la mapema ili kuwanyong’onyesha wapinzani wao.

Hali hiyo iliwafanya mabeki wa kila upande kufanya kazi ya ziada mara kwa mara kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani wasifanikiwe kutikisa nyavu ingawa hilo halikusaidia kwa asilimia mia moja kwani dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Yanga kutakata kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kila upande ulifanya mabadiliko kwa lengo la kujiongezea nguvu zaidi.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alimtoa Ngasa na kumwingiza Jafary Mohamed, akatoka Ibrahim Ajib na kumwingiza Pius Buswita na Amissi Tambwe, aliyetoka na kuingia Maka Edward.

Kwa upande wa Mbeya City alitoka  Eliud Ambokile na kuingia Peter Mapunda.

 Kipindi hiki pia timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu, Seleman na  Ambokile mara kadhaa walikuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini ukuta wa Yanga ukiongozwa na Kelvin Yondani, ulikuwa imara kuondosha mipira ya hatari.

Yanga kwa upande mwingine ilijibu kwa mashambulizi ya kushtukiza ambapo Makambo na Mohamed walipata nafasi nzuri lakini ukosefu wa umakini uliwafanya washindwe kuiandikia timu hiyo mabao zaidi.
Pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na kila upande, pambano hilo lilimalizika kwa Yanga kuondoka ugenini kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao Mbeya City.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo,  Azam FC iliangusha pointi zote tatu kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar  iliyokuwa nyumbani Uwanja wa Manungu.

Ruvu Shooting ikiwa nyumbani Uwanja wa Mabatini iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Biashara ya mkoani Mara, African Lyon na Mwadui zikatoka suluhu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Lipuli iliyolazimishwa suluhu na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Sokoine, Iringa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles