BARCELONA, HISPANIA
MSHAMBULIAJI wa pembeni wa timu ya Barcelona, Ousmane Dembele, ataukosa mchezo wa Ligi Kuu Hispania dhidi ya wapinzani wao Real Madrid ambao unajulikana kwa jina la El Clasico.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, ataukosa mchezo huo kutokana na kufungiwa michezo miwili baada ya kuoneshwa kadi nyekundu mwishoni mwa wiki iliopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Sevilla.
Katika mchezo huo, Barcelona walifanikiwa kushinda mabao 4-0, huku mchezaji huyo akifunga bao moja katika ushindi huo, lakini dakika ya 88 alioneshwa kadi nyekundu kutokana na kutoa kauli chafu kwa mwamuzi wa mchezo huo kwa kumwabia ‘Wewe ni mtu mbaya.’
Kauli hiyo aliitoa baada ya nyota wa Barcelona, Ronald Araujo kuoneshwa kadi nyekundu, hivyo wachezaji wawili wa Barcelona walioneshwa kadi hiyo.
Mwamuzi Antonio Mateu kupitia ripoti yake alisema kuwa, alitoa kadi hiyo kwa Dembele kutokana na mchezaji huyo kutumia kauli hiyo mara kwa mara, hivyo akaamua kumuonesha kadi hiyo.
Nahodha wa Barcelona, Lionel Messi, alijaribu kufanya mazungumzo na mwamuzi huyo akitaka kumsamehe Dembele kwa kuwa hajui kutamka vizuri maneno ya kihispania, lakini mwamuzi alifanya maamuzi yake sahihi.
Barcelona wanatarajia kuwa kwenye uwanja wa nyumbani Nou Camp kwa ajili ya kupambana na wapinzani wao Real Madrid, Oktoba 26, lakini Dembele mchezo mwingine ambao ataukosa ni dhidi ya Eibar, Oktoba 19.
Kukosekana kwa mchezaji huyo kwenye michezo hiyo mwili kutawapa nafasi wachezaji chipukizi Carles Perez mwenye umri wa miaka 21 na Ansu Fati mwenye miaka 16, kuwa kwenye kikosi hicho.
Makinda hao wameonesha kiwango cha hali ya juu tangu kuanza kwa msimu huu japokuwa wamekutana na changamoto za kugombania namba.