Neymar: Nipo tayari kuipigania PSG

0
690

PARIS, UFARANSA

MSHAMBULIAJI wa timu ya PSG, Neymar Jr, amefunguka na kusema kwa sasa ana furaha na amani kuwa ndani ya kikosi hicho, hivyo yupo tayari kuipigania timu hiyo.

Mshambuliaji huyo raia wa nchini Brazil, kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Septemba 2, alikuwa na lengo la kutaka kuondoka huku akihusishwa kuwindwa na klabu yaka ya zamani Barcelona pamoja na mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid, lakini dili hilo lilishindikana.

Kutokana na hali hiyo mashabiki wa PSG walikuwa wanamzomea mchezaji huyo mara baada ya kurudi kikosini msimu huu, lakini aliweza kuwanyamazisha mashabiki hao kwa kuifungia timu hiyo mabao manne kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu nchini Ufaransa.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Rio nchini Brazil wakati wa maandalizi wa mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Senegal, Neymar alisema lengo lake kubwa kwa sasa ni kuisaidia PSG.

“Kila mmoja ameona kilichotokea wakati wa soko la uhamisho majira haya ya kiangazi, ukweli ni kwamba nilikuwa na lengo la kutaka kuondoka PSG.

“Lakini baada ya kushindwa kuondoka bado nina furaha ya kuwa PSG, sisemi haya kwa kuwa nipo na timu ya taifa, ila naongea hivyo nimeona msimu huu umeanza vizuri kwangu, hivyo nipo tayari kuipigania kwa meno na kucha zangu. Nina asilimia 100 ya kuwa na mafanikio makubwa msimu huu.

“Kiangazi kilikuwa kirefu kwangu, lakini nilijiandaa kwa lolote, hivyo ninamshukuru Mungu msimu umeanza vizuri kwangu, ninaamini hali hii itaendelea hivi,” alisema Neymar.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alikuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu katika msimu wa 2018-19 kutokana na kusumbuliwa na mguu. Hivyo anaamini kwa sasa angekuwa bora zaidi endapo hasingepata majeraha hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here