Na Mwandishi Wetu, Tanga
Wadau wa sekta ya utalii na hoteli mkoani Tanga wametakiwa kuzingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi ikiwa ni mkakati mojawapo wa kujiandaa kunufaika na fursa mbali mbali za kiuchumi ukiwemo mradi mkubwa wa bomba la mafuta la Hoima-Tanga.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima katika ujumbe wake uliofikishwa kwa wadau hao kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja wakati akifungua kikao baina ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na wadau hao.
“Nitumie fursa hii kuwaeleza kwamba nyinyi kama wadau wa sekta ya utalii na hoteli mna mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwani sekta hii inashika nafasi ya pili baada ya sekta ya uzalishaji hivyo pamoja na umuhimu huo nilioueleza nitumie nafasi hii kuwasihi kuzingatia taratibu muhimu za afya na usalama mahali pa kazi,” ameeleza mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa.
Aliongeza: “Nadhani mmeshuhudia jitihada zinazofanywa na serikali ili kuinua sekta ya utalii iliyokuwa imeyumba kidogo kutokana na athari za janga la uviko-19. Jitahadi hizo zinaongozwa na Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan ambaye aliweza hata kushiriki katika filamu ya The Royal Tour yenye lengo la kutangaza vivutio vyetu vya utalii.
“Lakini pia amekuwa akifanya jitahadi nyingine nyingi za kuwavutia wawekezaji na hivyo kuzalisha fursa nyingi za kiuchumi ambazo endapo hatutaweza kufanya biashara zetu kwa kuzingatia sheria za nchi na viwango vya kimataifa ikiwemo masuala ya afya na usalama mahali pa kazi fursa hizi zitatupitia mbali,” amesema Masanja.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho, James Maurice, ameishukuru OSHA na kusema: “Kupitia kikao hiki tumepata fursa ya kujifunza na kujijenga zaidi hususan katika mambo tuliyokuwa hatuyafahamu jambo lilikuwa linapelekea kukwepa kuyatekeleza lakini tunaamini kwamba baada ya hapa tutakwenda kushirikiana vyema na OSHA,” amesema Maurice.
Mshiriki mwingine ambaye alijitambulisha kwa jina la Fatma Jokho amesema: “Tunashukuru kikao kimeenda vizuri, tumeweza kutoa maoni na kueleza changamoto zetu mbali mbali na tumetoa mapendekezo yetu ambayo tunaimani kwamba OSHA watayafanyia kazi,” amesema Fatma.
Kikao hicho kilichofanyika kwa siku mbili kimewahusisha wadau wa sekta za utalii na hoteli, usafirishaji, ujenzi, viwanda vidogo vidogo na madini ambapo mada mada mbali mbali zimewasilishwa na kujadiliwa ikiwemo dhana nzima ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Huduma za Ukaguzi mahali pa kazi pamoja na Upimaji Afya kwa wafanyakazi.
Miongoni mwa majukumu makuu ya OSHA ni kukuza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya miongoni mwa wadau na wananchi kwa ujumla ambapo kikao hiki imekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu hilo. Majukumu mengine ni pamoja na; Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, kufanya tafiti kuhusiana na masuala husika pamoja na kuishauri serikali kuhusiana na masuala ya Usalama na Afya ikiwemo uridhiaji wa mikataba ya Kimataifa.