27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

Osha bado inajukumu kutoa elimu kupunguza ajali kazini

FARAJA MASINDE

LENGO la Serikali inayongozwa na Rais Dk. John Magufuli, ni kuhakikisha uchumi wa nchi unaimarika hasusan kupitia viwanda.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa ukuaji wa sekta ya viwanda na kuimarisha uchumi, suala la usalama na afya kwenye mazingira ya kazi limekuwa ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha hali ya juu.

Hii ni kwa sababu kumekuwa kukiripotiwa matukio ya ajali mara kwa mara makazini kutokana na wahusika kutotimiza matakwa ya sheria na hivyo kugharimu maisha ya watu.

Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kupitia ripoti yake ya mwaka 2019 imebainisha kuwa watu 7,500 hufariki dunia kila siku kutokana na mazingira yasiyo salama na afya kazini.

Kama hiyo haitoshi, ILO kupitia ripoti hiyo inasema watu zaidi ya milioni 374 hujeruhiwa au kuugua kutokana na ajali kazini au kufanya kazi muda mrefu.

Pia imefafanua kuwa watu 6,500 hufariki kutokana na magonjwa yanayowapata kazini huku 1,000 wakifariki dunia kutokana na ajali kazini kiwago ambacho ni sawa na asilimia tano hadi saba ya vifo vyote vinavyotokea duniani.

Kwa upande wa hapa nchini, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), wamekuwa na mchango mkubwa kuhakikisha kunakuwapo mazingira salama kazini yanayosaidia kulinda nguvu kazi ya Taifa.

Osha ambao ni wakala wa serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), imepewa jukumu la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vilivyopo katika sehemu za kazi vinavyoweza kusababisha magonjwa, ajali na hata kifo ambapo imekuwa ikifanya hivyo kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, anasema lengo lao ni kuhakikisha wanazifikia sehemu nyingi za kazi kadri itakavyowezekana.

Anabainisha kuwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19 sehemu za kazi 16,457 zilisajiliwa na Osha ikilinganishwa na 3,354 zilizosajiliwa 2017/18 kabla ya kuondoa tozo, kiwango ambacho ni sawa na asilimia 491.

“Pia kaguzi 137,938 zilifanyika ukilinganisha na 85,491 zilizofanyika mwaka 2016/2017, sawa na ongezeko la asilimia 61.3. Hivyo, ongezeko hili katika usimamizi wa sheria linamaanisha sehemu nyingi za kazi zimefikiwa, kaguzi zimefanyika, tathmini ya afya imefanyika kwa wafanyakazi walio wengi na hivyo kuendelea kuimarisha hali ya usalama na afya mahali pa kazi,” anasema.

Mwenda anataja mafanikio mengine kuwa ni kuimarisha mifumo ya kiutendaji na usimamizi ndani ya taasisi, hali ambayo imesaidia kuondoa urasimu katika utoaji huduma na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji.

“Katika kufanikisha hili, tulifanya mapitio ya mlolongo wa biashara (Business Process Review) ili kubaini maeneo yanayoleta urasimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na kupitia mapitio hayo, Osha imefanikiwa kupunguza muda wa kutoa cheti cha usajili wa sehemu ya kazi kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na muda ya kushughulikia leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kutoka siku 28 hadi siku tatu baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu,” anasema.

Jukumu la Osha ni kupunguza ajali na magonjwa katika sehemu za kazi, lengo ambalo linatakiwa kwenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.

“Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, ilipendekeza kufutwa kwa tozo hizo ambapo Serikali iliridhia kufanya marekebisho kupitia GN. 719 ya Novemba 16, 2018 iliyofuta tozo mbalimbali zikiwamo ada ya usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh 50,000 hadi Sh 1, 800,000. Pia ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh 2,000 ilifutwa; faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto ya Sh 500,000 ambayo ilikuwa inaingiliana na taratibu zinazosimamiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” anasema Mwenda.

Kwa sasa, Osha ina ofisi katika kanda sita zinazohudumia nchi nzima ambazo ni Kanda ya Pwani (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro), Kanda ya Kati (Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza, Shinyinga, Simiyu, Mara, Geita na Kagera), Kanda ya Kaskazini (Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa, Njombe na Iringa) na Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma), huku majukumu yake makuu yakiwa ni manne.

Hata hivyo, Osha bado wanalojukumu kubwa la kuendelea kutoa elimu kwani kwa mujibu wa Utafiti wa kazi na Biashara wa Kituo cha Sheria na Haki za Bianadamu (LHRC) mwaka 2018/19, unaonyesha kuwa asilimia 37 ya wafanyakazi mahali pa kazi walisema hawajui utaratibu wa utoji fidia pindi ajali inapotokea mahala pa kazi, huku asilimia 35 wakikiri kwamba wanapata fidia inapotokea wameumia wakiwa kazini.

Asilimia 28 ya washiriki walidai kwamba hakuna utaratibu wa ulipaji fidia kazini.

Hata hivyo, wafanyakazi waliohojiwa katika baadhi ya mikoa kama vile Geita, Iringa, Njombe na Tanga walisema fidia inayotolewa ni ndogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles