Na Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imesema ongezeko la watu nchi halina athari za kiuchumi na kijamii kwa kuwa Tanzania ina rasilimali za kutosha kuhudumia watu wake kutokana na sera yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Susan Lyimo, aliyetaka ushauri wa Serikali kuhusu ongezeko la idadi ya watu lisiloendana na rasilimali zilizopo.
Dk. Kijaji alisema Serikali katika kuhakikisha ongezeko la watu linakuwa na faida kwa nchi, pamoja na mambo mengine imeanzisha miradi kama ufuaji wa umeme wa maji wa Mto Rufiji (Julius Nyerere), ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR lakini pia imeboresha huduma za afya, uimarishaji wa mtandao wa usafirishaji na elimu bure, mambo yanayochochea uanzishwaji wa viwanda vikubwa, vidogo na vya kati vitakavyo ajiri watanzania wengi.
“Mara zote idadi ya watu imekuwa na faida zaidi kwa nchi zinazoendelea ambazo teknolojia yake haijakua kwa kiasi kinachohitajika katika kuendeleza shughuli za kiuchumi ukilinganisha na nchi zilizoendelea duniani”, alieleza Dk. Kijaji.
Alisema rasilimali watu inaendelea kuongezeka kwa asilimia 2.7, idadi ambayo ni fursa ikizingatiwa kuwa ardhi ipo ya kutosha na Serikali ina uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa kuwa Tanzania imezungukwa na mito, mabwawa, bandari na rasilimali nyingine.
Alisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema, ili nchi iendelee inahitaji vitu vitatu ambavyo ni siasa safi, uongozi bora na watu.
Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na watu milioni 44.9 ilihali inamiliki rasilimali ardhi yenye eneo la kilomita za mraba 947,303 ambapo ardhi kavu ni 885,803 na eneo la maji ni 61,500 sawa na watu 65 kwa kila kilometa moja ya mraba kwa mwaka 2020, jambo linaloashiria idadi ya watu si tatizo nchini.
Aidha Dk. Kijaji alisema Seikli imeanza maandalizi ya awali kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwaka 2022.
Dk Kijaji alitoa rai ya kuhakikisha wananchi wanamuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa kuchapa kazi katika kuujenga uchumi wa viwanda ambao utasaidia kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.