25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kaliua watumia wanafunzi kumaliza upungufu wa madarasa, vyoo nyumba za walimu

NA ALLAN VICENT

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora, kwa kushirikiana na wanafunzi kupitia elimu ya kujitegemea imejenga vyumba vya madarasa 149, matundu ya vyoo 106 na nyumba za walimu 10. 

Kupitia elimu hiyo pia kila shule imepanda miti ya kivuli na matunda na kulima mazao mbalimbali ikiwemo korosho, mahindi, alizeti, viazi, karanga na mpunga, hivyo kuanzia mwakani watakula chakula shuleni. 

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Dk John Pima alisema mpango huo umeisaidia halmashauri kupunguza gharama za kutengeneza miundombinu katika shule zote ambapo imetumia Sh milioni 416.3 tu za mapato yake ya ndani kumalizia miradi hiyo.

Akizungumza katika kikao cha wataalamu na wadau wa elimu wilayani humo, alisema miundombinu hiyo imejengwa kutokana na ushirikiano mzuri baina kamati za maendeleo ya kata na vijiji, wazazi, wakuu wa shule, walimu na wanafunzi.

Alieleza ubunifu huo umewezesha wanafunzi wa shule zote kushiriki katika kazi za mikono baada ya muda wa masomo, ikiwa ni sehemu ya kujifunza stadi za maisha kwa vitendo ambapo hushiriki katika kazi za kufyatua tofali, kupanda miti na kilimo.

Dk Pima alisema dhana hiyo imekuwa na msaada mkubwa kwa kamati za maendeleo ya kata na vijiji ambapo hadi sasa matofari ya udongo milioni 2.573 yamefyatuliwa na kuchomwa.

Alisema kati matofali hayo, milioni 1.962 yalifyatuliwa na wanafunzi wa shule za msingi na 611, 216 wa shule za sekondari na ndio yametumika kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu katika shule zao.

Alisema wameweza kujenga vyumba 93 vya madarasa kwa shule za msingi, vyumba 56 kwa shule za sekondari, nyumba 11 za walimu wa elimu ya msingi, matundu 69 ya vyoo vya shule za msingi na 36 kwa shule za sekondari.

 Alisema kujengwa kwa miundombinu hiyo kumepunguza uhaba wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba vya walimu katika shule nyingi.

“Elimu ya kujitegemea imewapa watoto wetu uwezo, ujasiri, mbinu, ujuzi na uzalendo wa kweli, wakimaliza shule watakuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia wazazi wao kwenye kilimo na kufyatua tofali za kujengea nyumba”, alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles